Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 23:1-16

Yoshua 23:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya muda mrefu, Mwenyezi-Mungu aliwajalia Waisraeli amani kwa kuwaokoa na maadui zao pande zote. Wakati huo Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Yoshua aliwaita Waisraeli wote pamoja na viongozi na wazee wao, waamuzi na maofisa, akawaambia, “Sasa mimi nimekuwa mzee wa miaka mingi. Nyinyi mmeona mambo yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyoyatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye aliyewapigania. Nchi za mataifa yaliyobaki na yale niliyoyaangamiza nimewagawieni ziwe mali ya makabila yenu, kutoka Yordani mpaka bahari ya Mediteranea, upande wa magharibi. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawaondoa mbele yenu na kuwafukuza kabisa, nanyi mtaimiliki nchi yao kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi. Kwa hiyo, muwe imara katika kuzingatia yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose, kamwe msiyaache. Msishirikiane na mataifa haya yaliyobaki kati yenu. Msiitaje miungu yao wala msiape kwa majina ya miungu yao; msiitumikie wala msiisujudie. Bali ambataneni na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kama mlivyofanya mpaka leo. Maana Mwenyezi-Mungu ameyafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu na hakuna mtu ambaye ameweza kuwapinga nyinyi hadi leo. Mtu wenu mmoja tu anaweza kuwakimbiza maadui elfu, kwani Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye anayewapigania kama alivyowaahidi. Basi, muwe waangalifu sana kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana, kama mkimwasi Mwenyezi-Mungu na kujiunga na mataifa haya yaliyobaki kati yenu, mkaoa kwao nao wakaoa kwenu, jueni kwa hakika kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hataendelea kuyafukuza mataifa haya mbele yenu, bali yatakuwa kwenu kikwazo na mtego. Yatakuwa kwenu mjeledi wa kuwachapeni na miiba ya kuwachomeni machoni mpaka hapo mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. “Sasa, wakati wangu wa kufariki dunia kama ilivyo kawaida ya walimwengu wote umekaribia. Lakini nyinyi nyote mnajua wazi mioyoni na rohoni mwenu kwamba katika mambo yote mema ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wenu aliwaahidi, hakuna hata moja ambalo halikutimia. Yote yametimia kama vile alivyoahidi. Lakini kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyotimiza mambo yote mema aliyowaahidi, vivyo hivyo anaweza kuwaletea maovu yote mpaka awaangamize nyote kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni. Kama mkivunja agano lake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru mlishike, mkaenda kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, nanyi mtaangamia mara moja kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni.”

Shirikisha
Soma Yoshua 23

Yoshua 23:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata ikawa baada ya siku nyingi, BWANA alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli amani mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana, Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na waamuzi wao, na makamanda wao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimezeeka sana; nanyi mmeona mambo yote ambayo BWANA, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi. Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa makabila yenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa magharibi. Yeye BWANA, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama BWANA Mungu wenu, alivyowaambia. Basi, iweni thabiti sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kulia wala upande wa kushoto. Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao; bali shikamaneni na BWANA, Mungu wenu, kama mlivyotenda mpaka hivi leo. Maana BWANA amefukuza mbele yenu mataifa makuu na yenye nguvu, na kwenu ninyi hapana mtu aliyewahi kusimama mbele yenu hata leo. Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia. Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende BWANA, Mungu wenu. Lakini mkirudi nyuma kwa njia yoyote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya kuwa BWANA, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hadi mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi. Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena BWANA, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lolote mlilopungukiwa. Kisha itakuwa, kama yalivyowafikia yale mambo mema yote, BWANA, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika BWANA atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, BWANA Mungu wenu, aliyowapa. Hapo mtakapolivunja agano la BWANA, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya BWANA itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.

Shirikisha
Soma Yoshua 23

Yoshua 23:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ikawa baada ya siku nyingi, BWANA alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana, Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu; nanyi mmeona mambo yote ambayo BWANA, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi. Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua. Yeye BWANA, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama BWANA Mungu wenu, alivyowaambia. Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto. Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao; bali shikamaneni na BWANA, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo. Maana BWANA amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo. Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia. Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende BWANA, Mungu wenu. Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya kuwa BWANA, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi. Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena BWANA, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa. Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, BWANA, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika BWANA atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, BWANA Mungu wenu, aliyowapa. Hapo mtakapolivunja agano la BWANA, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya BWANA itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.

Shirikisha
Soma Yoshua 23

Yoshua 23:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya muda mrefu kupita, naye BWANA akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana. Ninyi wenyewe mmeona kila kitu BWANA Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni BWANA Mungu wenu aliyewapigania. Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi. BWANA Mungu wenu mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile BWANA Mungu wenu alivyowaahidi. “Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. Bali mtashikamana kwa uthabiti na BWANA, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa. “BWANA amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa BWANA Mungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi. Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda BWANA Mungu wenu. “Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, basi mwe na hakika kuwa BWANA Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, mpaka mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo BWANA Mungu wenu amewapa. “Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema BWANA Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. Lakini kama vile kila ahadi njema ya BWANA Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo BWANA ataleta maovu yote kama alivyo onya, mpaka awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. Kama mkilivunja agano la BWANA Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya BWANA itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”

Shirikisha
Soma Yoshua 23

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha