Yoshua 1:5-9
Yoshua 1:5-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe. Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa. Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote aliyokuamuru mtumishi wangu Mose. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe utafanikiwa popote uendapo. Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo. Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”
Yoshua 1:5-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hakuna mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda kulingana na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kulia, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda kulingana na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.
Yoshua 1:5-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.
Yoshua 1:5-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia. “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa BWANA Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”