Yona 3:6-10
Yona 3:6-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Habari hizi zikamfikia mfalme wa Ninewi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake rasmi, akajivika vazi la gunia na kuketi katika majivu. Kisha mfalme akawatangazia wakazi wa Ninewi: “Mimi mfalme, pamoja na wakuu wangu, natoa amri hii: Pasiwe na binadamu yeyote, ng'ombe au mnyama yeyote wa kufugwa, atakayeonja kitu chochote. Ni mwiko kwa mtu yeyote au mnyama kula au kunywa. Watu wote na wanyama wavae mavazi ya gunia. Kila mtu na amwombe Mungu na kumsihi kwa moyo. Naam, kila mmoja na aache uovu na ukatili wake. Huenda Mungu akabadili nia yake, akaacha kutukasirikia, tusije tukaangamia!” Mungu alipoona walivyofanya, na jinsi walivyouacha uovu wao, akabadili nia yake, akaacha kuwatenda kama alivyokuwa amekusudia.
Yona 3:6-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.
Yona 3:6-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.
Yona 3:6-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha enzi, akavua majoho yake ya kifalme, akajifunika nguo ya gunia kisha akaketi chini mavumbini. Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote: “Kwa amri ya mfalme na wakuu wake: “Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ngʼombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. Bali wanadamu na wanyama wafunikwe kwa nguo za gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.” Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.