Yona 2:1-9
Yona 2:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Yona akamwomba BWANA, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki, Akasema, Nalimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu; Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka shimoni, Ee BWANA, Mungu wangu, Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka BWANA; Maombi yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu. Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe; Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa BWANA.
Yona 2:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema: “Kwa sababu ya taabu yangu, nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu, nawe ukanisikiliza; toka chini kuzimu, nilikulilia, nawe ukasikiliza kilio changu. Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari, gharika ikanizunguka, mawimbi na gharika vikapita juu yangu. Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako; nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu. Maji yalinizunguka na kunisonga; kilindi kilinifikia kila upande, majani ya baharini yakanifunika kichwa. Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima, katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umenipandisha hai kutoka humo shimoni. Roho yangu ilipoanza kunitoka, nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, sala yangu ikakufikia, katika hekalu lako takatifu. Watu wanaoabudu sanamu za miungu batili, huutupilia mbali uaminifu wao kwako. Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea sadaka, na kutimiza nadhiri zangu. Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye.”
Yona 2:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Yona akamwomba BWANA, Mungu wake, akiwa katika tumbo la yule samaki, Akasema, Nilimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu niliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu; Nilishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi ambayo mapingo yake yanafunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka humo shimoni, Ee BWANA, Mungu wangu, Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nilimkumbuka BWANA; Maombi yangu yakakufikia, Katika hekalu lako takatifu. Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe. Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa BWANA.
Yona 2:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba BWANA Mungu wake. Akasema: “Katika shida yangu nalimwita BWANA, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu. Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka, mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu. Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’ Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu. Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee BWANA Mungu wangu. “Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, BWANA, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu. “Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao. Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea dhabihu. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa BWANA.”