Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yona 1:1-17

Yona 1:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yona, mwana wa Amitai: “Ondoka uende Ninewi, ule mji mkuu, ukaukemee, maana nimeona uovu wake ni mkubwa mno.” Basi, Yona akaanza safari, lakini akashika njia ya kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Akaenda hadi mjini Yopa ambapo alikuta meli moja iko tayari kwenda Tarshishi. Alilipa nauli, akapanda meli, akasafiri na mabaharia hao kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika. Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito. Nahodha akamwendea, akamwambia, “Wawezaje wewe kulala? Amka umwombe Mungu wako; labda Mungu wako atatuhurumia, tusiangamie.” Mabaharia wakasemezana: “Tupige kura tujue balaa hili limetupata kwa kosa la nani.” Basi, wakapiga kura; kura ikamwangukia Yona. Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?” Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.” Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!” Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?” Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.” Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia. Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.” Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia. Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaamuru samaki mkubwa ammeze Yona, naye akawa tumboni mwa samaki huyo kwa muda wa siku tatu, usiku na mchana.

Shirikisha
Soma Yona 1

Yona 1:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akateremka hadi Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akalipa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA. Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu kuvunjika. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hadi pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na tupige kura, tupate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewaambia. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; kisha bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana. Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. Ndipo wale watu wakamwogopa BWANA mno, wakamtolea BWANA sadaka, na kuweka nadhiri. BWANA akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.

Shirikisha
Soma Yona 1

Yona 1:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA. Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewajulisha. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana. Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. Ndipo wale watu wakamwogopa BWANA mno, wakamtolea BWANA sadaka, na kuweka nadhiri. BWANA akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.

Shirikisha
Soma Yona 1

Yona 1:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA lilimjia Yona mwana wa Amitai: “Nenda katika mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri juu yake, kwa sababu uovu wake umekuja juu mbele zangu.” Lakini Yona alimkimbia BWANA na kuelekea Tarshishi. Alishuka mpaka Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda melini na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia BWANA. Ndipo BWANA akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini kuvunjika. Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito. Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, mahali ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito. Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.” Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, kura ikamwangukia Yona. Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?” Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu BWANA, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.” Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza, “Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia BWANA, kwa sababu alishawaambia hivyo.) Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?” Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.” Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia wawezavyo ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo. Ndipo wakamlilia BWANA, “Ee BWANA, tafadhali usituue kwa kuondoa uhai wa mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kuutoa uhai wa mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee BWANA, umefanya kama ilivyokupendeza.” Kisha walimchukua Yona, wakamtupa baharini nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia. Katika jambo hili watu wakamwogopa BWANA sana, wakamtolea BWANA dhabihu na kumwekea nadhiri. Lakini BWANA akamwandaa nyangumi kummeza Yona, naye Yona alikuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana.

Shirikisha
Soma Yona 1