Yoeli 1:13-20
Yoeli 1:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza, lieni enyi wahudumu wa madhabahu. Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha! Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu. Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi, nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu. Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu, siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia; inakuja pamoja na maangamizi, kutoka kwa Mungu Mkuu. Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama. Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu. Mbegu zinaoza udongoni; ghala za nafaka ni ukiwa mtupu, ghala zimeharibika, kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi. Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni! Makundi ya ng'ombe yanahangaika, kwa sababu yamekosa malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka. Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, moto umemaliza malisho nyikani, miali ya moto imeteketeza miti mashambani. Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe, maana, vijito vya maji vimekauka, moto umemaliza malisho nyikani.
Yoeli 1:13-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njooni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA, Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya BWANA inakaribia, nayo itakuja kama maangamizi yatokayo kwake aliye Mwenyezi. Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; mabohari yameachwa ukiwa; ghala zimeharibika; kwa maana nafaka imekauka. Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng'ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamehangaika. Ee BWANA, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba. Naam, hata wanyama pori wanakulilia wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.
Yoeli 1:13-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA, Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya BWANA inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye Mwenyezi. Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka. Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng’ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamepata mateso. Ee BWANA, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba. Naam, wanyama wa mashamba wanakutwetea wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.
Yoeli 1:13-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Vaeni gunia, enyi makuhani, mwomboleze; pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. Njooni, vaeni gunia usiku kucha, enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu. Tangazeni saumu takatifu; liiteni kusanyiko takatifu. Waiteni wazee na wote wanaoishi katika nchi waende katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, wakamlilie Mwenyezi Mungu. Ole kwa siku hiyo! Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu; itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi. Je, chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu: furaha na shangwe kutoka nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinakauka chini ya mabonge ya udongo. Maghala yameachwa katika uharibifu, maghala ya nafaka yamebomolewa, kwa maana hakuna nafaka. Jinsi gani ng’ombe wanavyolia! Makundi ya mifugo yanahangaika kwa sababu hawana malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka. Kwako, Ee Mwenyezi Mungu, naita, kwa kuwa moto umeteketeza malisho ya mbugani na miali ya moto imeunguza miti yote shambani. Hata wanyama pori wanakuonea shauku; vijito vya maji vimekauka, na moto umeteketeza malisho yote ya mbugani.