Yobu 42:1-6
Yobu 42:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu: “Najua kwamba waweza kila kitu, lolote unalokusudia haliwezi kuzuiliwa. Ulisema kuwa nilithubutu kutatiza mpango wako kijinga. Kweli nilitamka kitu ambacho sikuelewa mambo ya ajabu mno kwangu ambayo sikuwa ninayajua. Uliniambia nisikilize nawe utaniambia; kwamba utaniuliza nami nikujibu. Kweli nilikuwa nimesikia habari zako kwa masikio tu, lakini sasa nakuona kwa macho yangu mwenyewe. Kwa hiyo natubu pamoja na kujipaka mavumbi na majivu, najiona mimi mwenyewe kuwa si kitu kabisa.”
Yobu 42:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema. Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye ushauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu.
Yobu 42:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema. Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu.
Yobu 42:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Ayubu akamjibu BWANA: “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote, wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika. Uliuliza, ‘Ni nani huyu afichaye mashauri yangu bila maarifa?’ Hakika nilisema juu ya mambo niliyokuwa siyaelewi, mambo ya ajabu mno kwangu mimi kuyajua. “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena; nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’ Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako, lakini sasa macho yangu yamekuona. Kwa hiyo najidharau mwenyewe, na kutubu katika mavumbi na majivu.”