Yobu 29:1-10
Yobu 29:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema, Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya kale, Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda; Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani, Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake; Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu; Wakati Mwenyezi alipokuwa akali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka; Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta! Wakati nilipotoka kwenda mjini, hata langoni, Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu, Hao vijana waliniona wakajificha, Nao wazee wakaniondokea na kusimama; Wakuu wakanyamaa wasinene, Na kuweka mikono yao vinywani mwao; Sauti yao masheki ilinyamaa, Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao.
Yobu 29:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akaendelea na hoja yake, akasema: “Laiti ningekuwa kama zamani, wakati ule ambapo Mungu alinichunga; wakati taa yake iliponiangazia kichwani, na kwa mwanga wake nikatembea gizani. Wakati huo nilifikia ukamilifu wa maisha, wakati urafiki wa Mungu ulikaa nyumbani kwangu. Mungu Mwenye Nguvu alikuwa bado pamoja nami, na watoto wangu walinizunguka. Nyakati hizo niliogelea kwenye ufanisi, miamba ilinitiririshia vijito vya mafuta! Nilipokutana na wazee langoni mwa mji na kuchukua nafasi yangu mkutanoni, vijana waliponiona walisimama kando, na wazee walisimama wima kwa heshima. Wakuu waliponiona waliacha kuzungumza waliweka mikono juu ya midomo kuwataka watu wakae kimya. Sauti za waheshimiwa zilinyamazishwa, na vinywa vyao vikafumbwa.
Yobu 29:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Ayubu akaendelea na hoja yake, na kusema, Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya zamani, Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda; Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani, Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake; Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu; Wakati Mwenyezi alipokuwa angali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka; Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta! Wakati nilipotoka kwenda mjini, kupitia langoni, Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu, Hao vijana waliniona wakanipisha, Nao wazee wakasimama kwa heshima; Wakuu wakanyamaa wasinene, Na kuweka mikono yao vinywani mwao; Sauti yao wakuu ilinyamaa, Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao.
Yobu 29:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita, zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda, wakati taa yake iliniangazia kichwani changu, na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza! Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu, wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu, wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami, nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka, wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi, nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni. “Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji na kuketi katika kiwanja, vijana waliniona wakakaa kando, nao wazee walioketi wakasimama; wakuu wakaacha kuzungumza na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao; wenye vyeo wakanyamazishwa, nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.