Yobu 23:1-9
Yobu 23:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akajibu: “Leo pia lalamiko langu ni chungu. Napata maumivu na kusononeka. Laiti ningejua mahali nitakapompata Mungu! Ningeweza kwenda hata karibu naye. Ningeleta kesi yangu mbele yake, na kumtolea hoja yangu. Ningeweza kujua atakachonijibu, na kuelewa atakachoniambia. Je, angeshindana nami kwa nguvu zake zote? La! Bila shaka angenisikiliza. Yeye aweza kuzungumza na mtu mnyofu, Mungu, hakimu wangu angeamua kuwa sina hatia milele. “Tazama, nakwenda mbele, lakini simpati, narudi nyuma, lakini siwezi kumwona. Namtafuta upande wa kushoto lakini simwoni; nageukia kulia, lakini siwezi kumwona.
Yobu 23:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Hata leo malalamiko yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu. Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka kesi yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza. Hapo waelekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kulia, hata nisimwone.
Yobu 23:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu. Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza. Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.
Yobu 23:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Ayubu akajibu: “Hata leo malalamiko yangu ni chungu; mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua. Laiti ningefahamu mahali pa kumwona; laiti ningeweza kwenda mahali akaapo! Ningeliweka shauri langu mbele zake, na kukijaza kinywa changu na hoja. Ningejua kwamba angenijibu nini, na kuelewa lile ambalo angelisema. Je, angenipinga kwa nguvu nyingi? La, asingenigandamiza. Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake, nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu. “Lakini nikienda mashariki, hayupo; nikienda magharibi, simpati. Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni; akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.