Yobu 23:1-17
Yobu 23:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akajibu: “Leo pia lalamiko langu ni chungu. Napata maumivu na kusononeka. Laiti ningejua mahali nitakapompata Mungu! Ningeweza kwenda hata karibu naye. Ningeleta kesi yangu mbele yake, na kumtolea hoja yangu. Ningeweza kujua atakachonijibu, na kuelewa atakachoniambia. Je, angeshindana nami kwa nguvu zake zote? La! Bila shaka angenisikiliza. Yeye aweza kuzungumza na mtu mnyofu, Mungu, hakimu wangu angeamua kuwa sina hatia milele. “Tazama, nakwenda mbele, lakini simpati, narudi nyuma, lakini siwezi kumwona. Namtafuta upande wa kushoto lakini simwoni; nageukia kulia, lakini siwezi kumwona. Lakini yeye anajua njia ninayofuata; atakapomaliza kunijaribu nitatoka humo safi kama dhahabu. Nafuata nyayo zake kwa uaminifu njia yake nimeishikilia wala sikupinda. Kamwe sijaacha kushika amri yake, maneno yake nimeyatunza moyoni mwangu. Lakini yeye habadiliki, nani awezaye kumgeuza? Analotaka, ndilo analofanya! Atanijulisha yote aliyonipangia; na mengi kama hayo yamo akilini mwake. Hivyo, natetemeka kwa hofu mbele yake; hata nikifikiria tu napatwa na woga. Mungu ameufanya moyo wangu ufifie, Mungu Mwenye Nguvu amenitia hofu. Maana nimekumbwa na giza, na giza nene limetanda usoni mwangu.
Yobu 23:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Hata leo malalamiko yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu. Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka kesi yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza. Hapo waelekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kulia, hata nisimwone. Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu, Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo. Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye. Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa. Kwa maana Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha; Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.
Yobu 23:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu. Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza. Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone. Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu, Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo. Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye. Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa. Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha; Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.
Yobu 23:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Ayubu akajibu: “Hata leo malalamiko yangu ni chungu; mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua. Laiti ningefahamu mahali pa kumwona; laiti ningeweza kwenda mahali akaapo! Ningeliweka shauri langu mbele zake, na kukijaza kinywa changu na hoja. Ningejua kwamba angenijibu nini, na kuelewa lile ambalo angelisema. Je, angenipinga kwa nguvu nyingi? La, asingenigandamiza. Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake, nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu. “Lakini nikienda mashariki, hayupo; nikienda magharibi, simpati. Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni; akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo. Lakini anaijua njia niiendeayo; akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu; nimeishika njia yake bila kukengeuka. Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake; nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku. “Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga? Yeye hufanya lolote atakalo. Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu, na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba. Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake; nifikiriapo haya yote ninamwogopa. Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia; yeye Mwenyezi amenitia hofu. Hata hivyo sijanyamazishwa na giza, wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.