Yobu 1:1-22
Yobu 1:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng’ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote. Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA. Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng’ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.
Yobu 1:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Palikuwa na mtu mmoja nchini Usi, aitwaye Yobu. Mtu huyo alikuwa mwema na mnyofu; mtu mcha Mungu na mwenye kuepukana na uovu. Yobu alikuwa na watoto saba wa kiume na watatu wa kike; alikuwa na kondoo 7,000, ngamia 3,000, jozi 500 za ng'ombe na punda majike 500; na watumishi wengi sana; yeye alikuwa mashuhuri kuliko watu wote huko mashariki. Mara kwa mara, wanawe Yobu walifanya karamu nyumbani kwa kila mmoja wao kwa zamu; waliwaalika dada zao kula na kunywa pamoja nao. Kila baada ya karamu, Yobu aliwaita wanawe ili awatakase. Aliamka asubuhi na mapema baada ya karamu, akatoa tambiko za kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao kwani aliwaza, “Huenda wanangu wametenda dhambi na kumtukana Mungu mioyoni mwao.” Basi, ikatokia siku moja malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani, akajitokeza pia pamoja nao. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Bila shaka umemtambua mtumishi wangu Yobu. Duniani kote hamna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu.” Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Je, Yobu anamcha Mwenyezi-Mungu bure? Je, si dhahiri kwamba wewe unamlinda pande zote pamoja na jamaa yake na kila kitu alicho nacho? Wewe umembariki na mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini sasa, hebu nyosha tu mkono wako uiguse mali yake kama hutaona akikutukana waziwazi!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya, waweza kufanya chochote uwezacho juu ya mali yake; ila tu yeye mwenyewe usimguse.” Basi, Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ikawa siku moja, watoto wa kiume na wa kike wa Yobu walikuwa wanakula na kunywa pamoja nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Basi, mtumishi akafika kwa Yobu, akamwambia, “Tulikuwa tunalima kwa majembe ya kukokotwa na ng'ombe. Punda nao walikuwa wanakula hapo karibu. Basi Wasabea wakatuvamia na kuwachukua wanyama na kuwaua watumishi kwa upanga. Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Umeme wa radi umewachoma na kuwateketeza kondoo na watumishi, mimi tu peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Huyo naye kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Wakaldayo walijipanga makundi matatu wakashambulia ngamia, wakawachukua, na kuwaua watumishi wako kwa upanga! Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, akaja mwingine, akasema, “Watoto wako wa kiume na wa kike walikuwa wanakula na kunywa divai nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Mara kimbunga kikavuma kutoka jangwani, kikaipiga nyumba hiyo kila upande nayo ikawaangukia, na vijana wote wamekufa, mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kisha Yobu akasimama, akararua mavazi yake, akanyoa nywele zake, akajitupa chini na kumwabudu Mungu. Akasema, “Uchi nilikuja duniani, uchi nitaondoka duniani; Mwenyezi-Mungu amenipa, Mwenyezi-Mungu amechukua; litukuzwe jina lake Mwenyezi-Mungu.” Katika mambo haya yote Yobu hakutenda dhambi wala hakumfikiria Mungu kuwa ana kosa.
Yobu 1:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake watoto saba wa kiume, na binti watatu. Mali yake nayo ilikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watumishi wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe wa kiume huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakawaalika dada zao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Pengine hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote. Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujiweka mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu anamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA. Ilitukia siku moja hao watoto wake wa kiume na kike walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakila karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao wa kiume na wa kike walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nikiwa uchi, nami nitarudi tena huko uchi vile vile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.
Yobu 1:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu. Alikuwa na wana saba na binti watatu, naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu mkuu sana miongoni mwa watu wa Mashariki. Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika umbu zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao. Wakati kipindi cha karamu kilimalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu. Siku moja wana wa Mungu walikwenda kujionyesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao. BWANA akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu BWANA, “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.” Ndipo BWANA akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.” Shetani akamjibu BWANA, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? Je, wewe hukumjengea boma pande zote yeye na wa nyumbani mwake pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.” BWANA akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini juu ya huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.” Ndipo Shetani akatoka mbele za BWANA. Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari.” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako na binti zako walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!” Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu na kusema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi, nami nitaondoka uchi, BWANA alinipa, naye BWANA ameviondoa, jina la BWANA litukuzwe.” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.