Yohane 8:31-38
Yohane 8:31-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.” Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: ‘Mtakuwa huru?’” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. Mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. Najua kwamba nyinyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamyakubali mafundisho yangu. Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”
Yohane 8:31-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Abrahamu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wowote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Abrahamu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.
Yohane 8:31-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.
Yohane 8:31-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.” Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”