Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 7:25-44

Yohane 7:25-44 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?” Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’” Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado). Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:25-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Inawezekana hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenituma ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma. Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu? Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate. Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja. Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda kwa Utawanyiko wa Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja? Katika siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema kuhusu Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:25-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma. Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado. Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu? Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung’unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate. Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka. Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja. Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda kwa Utawanyiko wa Wayunani, na kuwafundisha Wayunani? Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja? Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:25-44 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? Mbona yuko hapa anazungumza hadharani na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo? Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.” Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.” Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu zaidi kuliko aliyoifanya mtu huyu?” Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata. Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.” Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?” Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa. Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya? Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu. Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

Shirikisha
Soma Yohane 7

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha