Yohane 5:24-40
Yohane 5:24-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenituma ana uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa inakuja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenituma. Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli. Si kwamba ninaupokea ushuhuda wa wanadamu; lakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung'aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkuu kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenituma amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mnayachunguza maandiko kwa sababu mnadhani kuwa ndani yake ninyi mna uzima wa milele; na maandiko yayo hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.
Yohane 5:24-40 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai. Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi. Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai. Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu. Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa. “Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai.
Yohane 5:24-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.
Yohane 5:24-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani. Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai. Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu. “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe. “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli. “Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli. Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa. Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake. “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye alinituma. Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.