Yohane 4:1-42
Yohane 4:1-42 Biblia Habari Njema (BHN)
Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane. (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.) Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya; na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria. Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu). Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekuambia: ‘Nipatie maji ninywe,’ ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yenye uhai.” Huyo mama akasema, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yenye uhai? Au, labda wewe wajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo wake walikunywa maji ya kisima hiki.” Yesu akamjibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uhai na kumpatia uhai wa milele.” Huyo mwanamke akamwambia, “Bwana, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; na, nisije tena mpaka hapa kuteka maji.” Yesu akamwambia, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume. Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.” Huyo Mwanamke akamwambia, “Bwana, naona ya kuwa wewe u nabii. Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini nyinyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudia Mungu ni kule Yerusalemu.” Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. Nyinyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.” Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.” Yesu akamwambia, “Mimi ninayeongea nawe, ndiye.” Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?” Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu, “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?” Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu. Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.” Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?” Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake. Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa. Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uhai wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna.’ Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho; wengine walifanya kazi, lakini nyinyi mnafaidika kutokana na jasho lao.” Wasamaria wengi wa kijiji kile walimwamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.” Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. Watu wengi zaidi waliamini kwa sababu ya ujumbe wake. Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.”
Yohane 4:1-42 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake) aliondoka Yudea, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. Basi akafika katika mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawatangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; lakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka. Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye. Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Inawezekana kuwa huyu ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenituma, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yanakuja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi niliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena tunajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.
Yohane 4:1-42 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,) aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka. Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye. Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.
Yohane 4:1-42 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mafarisayo wakasikia kwamba Yesu alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yohana, ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya. Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yosefu. Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.) Yesu akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.” Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?” Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.” Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!” Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.” Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.” Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Kristo) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.” Yesu akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.” Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?” Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu, “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Kristo?” Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Yesu. Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.” Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.” Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.” Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini. Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”