Yohane 2:18-25
Yohane 2:18-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, “Utafanya mwujiza gani kuonesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?” Yesu akawaambia, “Vunjeni hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu.” Hapo Wayahudi wakasema, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arubaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?” Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya hekalu ambalo ni mwili wake. Basi, alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakayaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno ambayo Yesu alikuwa amesema. Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizofanya. Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote. Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.
Yohane 2:18-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuoneshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arubaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.
Yohane 2:18-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.
Yohane 2:18-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?” Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!” Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema. Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakaamini katika jina lake. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote. Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.