Yohane 16:28-33
Yohane 16:28-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba. Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa? Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.
Yohane 16:28-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni, sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.” Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo. Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”
Yohane 16:28-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.” Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa? Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo nyinyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Yohane 16:28-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba. Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yoyote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa? Tazama, saa inakuja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; lakini mimi siko peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.