Yohane 12:35-46
Yohane 12:35-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Nendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako. Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone. Lakini ingawa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Lakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenituma. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenituma. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.
Yohane 12:35-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako. Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone. Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.
Yohane 12:35-46 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?” Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena: “Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya.” Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.
Yohane 12:35-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda. Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone. Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.” Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake. Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu. Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.