Yohane 12:12-19
Yohane 12:12-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema: “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli.” Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko: “Usiogope mji wa Siyoni! Tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwanapunda!” Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia. Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”
Yohane 12:12-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nayo kesho yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu; wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli! Naye Yesu alikuwa amepata mwanapunda, akampanda, kama vile iliyoandikwa, Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwanapunda. Mambo hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo. Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua. Na kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo. Basi Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lolote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.
Yohane 12:12-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nayo siku ya pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu; wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli! Naye Yesu alikuwa amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa, Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda. Mambo hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo. Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua. Na kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo. Basi Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.
Yohane 12:12-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu. Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!” Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa, “Usiogope, Ewe binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda!” Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye. Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia. Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki. Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”