Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 10:1-19

Yohane 10:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu. Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

Shirikisha
Soma Yohane 10

Yohane 10:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

“Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyanganyi. Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. Mngojamlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake, na kuwaongoza nje. Akisha watoa nje huwatangulia mbele, nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake.” Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. Basi, akasema tena, “Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyanganyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai – uhai kamili. “Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. “Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. Hakuna mtu anayeninyanganya uhai wangu; mimi nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye.” Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.

Shirikisha
Soma Yohane 10

Yohane 10:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwizi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wezi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwizi huja tu kuiba, kuua na kuharibu; mimi nilikuja ili wawe na uzima, tena wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nililipokea kwa Baba yangu. Kukawa na utengano tena kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

Shirikisha
Soma Yohane 10

Yohane 10:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwizi na mnyangʼanyi. Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia. Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.” Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika.

Shirikisha
Soma Yohane 10