Yeremia 3:1-5
Yeremia 3:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mume akimpa talaka mkewe, naye akaondoka kwake, na kuwa mke wa mwanamume mwingine, je mume yule aweza kumrudia mwanamke huyo? Je, kufanya hivyo hakutaitia nchi unajisi mkubwa? Wewe Israeli, umefanya ukahaba na wapenzi wengi, je, sasa unataka kunirudia mimi? Inua macho uvitazame vilele vya vilima! Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe? Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia, kama bedui aviziavyo watu jangwani. Umeifanya nchi kuwa najisi, kwa ukahaba wako mbaya kupindukia. Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa, na wala mvua za vuli hazijanyesha. Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba, huna haya hata kidogo. “Hivi punde tu si ulinililia ukisema: ‘Wewe u baba yangu, ulinipenda tangu utoto wangu? Je, utanikasirikia daima? Utachukizwa nami milele?’ Israeli, hivyo ndivyo unavyosema; na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.”
Yeremia 3:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Watu husema, Mtu akimwacha mkewe, naye akienda zake, akawa mke wa mtu mwingine, je! Mtu huyo atamrudia tena? Je! Nchi hiyo haitatiwa unajisi? Lakini wewe umefanya mambo ya ukahaba na wapenzi wengi; nawe, je! Utanirudia mimi? Asema BWANA. Inua macho yako, ukavitazame vilele vya milima, ukaone; pako wapi mahali ambapo hawakulala nawe? Kando ya njia umeketi ili kuwangojea, kama vile Mwarabu jangwani; nawe umeitia nchi unajisi kwa ukahaba wako na uovu wako. Kwa sababu hiyo manyunyu yamezuiliwa, wala hapakuwa na mvua ya vuli; hata hivyo ulikuwa na kipaji cha uso cha kahaba, ulikataa kutahayarika. Je, tokea wakati huu hutanililia, Ee Baba yangu, wewe u kiongozi wa ujana wangu? Je! Ataishika hasira yake hata milele? Ataishika hata mwisho? Tazama, umesema hivyo, bali umetenda mambo mabaya, umefuata njia yako mwenyewe.
Yeremia 3:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Watu husema, Mtu akimwacha mkewe, naye akienda zake, akawa mke wa mtu mwingine, je! Mtu huyo atamrudia tena? Je! Nchi hiyo haitatiwa unajisi? Lakini wewe umefanya mambo ya ukahaba na wapenzi wengi; nawe, je! Utanirudia mimi? Asema BWANA. Inua macho yako, ukavitazame vilele vya milima, ukaone; pa wapi mahali ambapo hawakulala nawe? Kando ya njia umeketi ili kuwangojea, kama vile Mwarabu jangwani; nawe umeitia nchi unajisi kwa ukahaba wako na uovu wako. Kwa sababu hiyo manyunyu yamezuiliwa, wala hapakuwa na mvua ya vuli; hata hivyo ulikuwa na kipaji cha uso cha kahaba, ulikataa kutahayarika. Je, tokea wakati huu hutanililia, Ee Baba yangu, wewe u kiongozi wa ujana wangu? Je! Ataishika hasira yake hata milele? Ataishika hata mwisho? Tazama, umesema hivyo, bali umetenda mambo mabaya, umefuata njia yako mwenyewe.
Yeremia 3:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kama mtu akimpa talaka mkewe, naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine, je, huyo mume aweza kumrudia tena? Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa? Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi: je, sasa utanirudia tena?” asema BWANA. “Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone. Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe? Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi, ukakaa kama yeye ahamahamaye jangwani. Umeinajisi nchi kwa ukahaba wako na uovu wako. Kwa hiyo mvua imezuiliwa, nazo mvua za vuli hazikunyesha. Hata hivyo, una uso usio na haya kama wa kahaba; unakataa kutahayari kwa aibu. Je, wewe hujaniita hivi punde tu: ‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu, je, utakasirika siku zote? Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’ Hivi ndivyo unavyozungumza, lakini unafanya maovu yote uwezayo.”