Yeremia 29:1-7
Yeremia 29:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno haya ndiyo maneno ya barua, ambayo nabii Yeremia alituma toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadneza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hadi Babeli; (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;) kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hadi Babeli, kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli), kusema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli; Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake; oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue. Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa BWANA; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.
Yeremia 29:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu. (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.) Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema: Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake. Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake, nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue. Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni BWANA kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
Yeremia 29:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Ifuatayo ni barua ambayo nabii Yeremia aliwapelekea kutoka Yerusalemu wazee na makuhani, manabii na watu ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kutoka Yerusalemu akawapeleka uhamishoni Babuloni. Yeremia aliiandika barua hiyo baada ya mfalme Yekonia na mama mfalme, matowashi, wakuu wa Yuda na Yerusalemu, mafundi na wahunzi kuondoka Yerusalemu. Barua hii ilipelekwa na Elasa mwana wa Shafani, na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Yeremia aliandika hivi: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kuhusu mateka wote aliowaacha wachukuliwe kutoka Yerusalemu hadi Babuloni: ‘Jengeni nyumba mkae. Limeni mashamba, pandeni mbegu na kula mazao yake. Oeni wake, mpate watoto; waozeni wana wenu na binti zenu nao pia wapate watoto. Ongezekeni na wala msipungue. Shughulikieni ustawi wa mji ambamo nimewahamishia. Niombeni kwa ajili ya mji huo, maana katika ustawi wake nyinyi mtastawi.
Yeremia 29:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli; (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;) kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hata Babeli, kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli), kusema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli; Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake; oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue. Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa BWANA; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.