Yeremia 29:1-31
Yeremia 29:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Ifuatayo ni barua ambayo nabii Yeremia aliwapelekea kutoka Yerusalemu wazee na makuhani, manabii na watu ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kutoka Yerusalemu akawapeleka uhamishoni Babuloni. Yeremia aliiandika barua hiyo baada ya mfalme Yekonia na mama mfalme, matowashi, wakuu wa Yuda na Yerusalemu, mafundi na wahunzi kuondoka Yerusalemu. Barua hii ilipelekwa na Elasa mwana wa Shafani, na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Yeremia aliandika hivi: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kuhusu mateka wote aliowaacha wachukuliwe kutoka Yerusalemu hadi Babuloni: ‘Jengeni nyumba mkae. Limeni mashamba, pandeni mbegu na kula mazao yake. Oeni wake, mpate watoto; waozeni wana wenu na binti zenu nao pia wapate watoto. Ongezekeni na wala msipungue. Shughulikieni ustawi wa mji ambamo nimewahamishia. Niombeni kwa ajili ya mji huo, maana katika ustawi wake nyinyi mtastawi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Msikubali kudanganywa na manabii wenu na waaguzi waliomo miongoni mwenu, wala msisikilize ndoto wanazoota. Maana wanawatabiria uongo kwa kutumia jina langu. Mimi sikuwatuma. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’ “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka sabini huko Babuloni, baada ya muda huo, nitawajia na kuitimiza ahadi yangu ya kuwarudisha mahali hapa. Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye. Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kunipata. Mtakaponitafuta kwa moyo wote mtanipata. Nami nitawarudishieni fanaka zenu na kuwakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipowafukuzia. Nitawarudisheni mahali ambapo niliwatoa, nikawapeleka uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nyinyi mnawasadiki manabii ambao mwasema kwamba Mwenyezi-Mungu amewaleteeni huko Babuloni. Sikilizeni nisemavyo mimi Mwenyezi-Mungu kuhusu mfalme anayekalia kiti cha enzi cha Daudi, na kuhusu watu wote wanaokaa katika mji huu, na ndugu zenu ambao hawakuondoka pamoja nanyi kwenda uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Tazama, ninawapelekea upanga, njaa na maradhi mabaya; nitawafanya kuwa kama tini mbaya sana, hata haziwezi kuliwa. Nitawaandama kwa upanga, njaa na maradhi mabaya. Nitawafanya kuwa kitu cha kuchukiza kwa tawala zote za dunia, naam, kitu cha laana, kioja, dharau na kitu cha kupuuzwa katika mataifa yote nilikowafukuzia. Nitafanya hivyo kwa sababu hamkusikiliza maneno yangu niliyowaambia kila mara kwa njia ya watumishi wangu, manabii, nanyi mkakataa kusikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Enyi nyote niliowatoa kutoka Yerusalemu, nikawapeleka uhamishoni Babuloni, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi juu ya Ahabu mwana wa Kolaya, na juu ya Sedekia mwana wa Maaseya, ambao wanawatabirieni uongo kwa jina lake: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, naye atawaua mkiona kwa macho yenu wenyewe. Kwa sababu jambo hilo litakalowapata, watu wote waliohamishiwa Babuloni kutoka Yerusalemu watatumia msemo huu wa kulaania: Mwenyezi-Mungu akufanye kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babuloni aliwachoma motoni. Kisa ni kwamba walitenda mambo ya aibu katika Israeli. Walizini na wake za jirani zao, na kusema maneno ya uongo kwa jina langu, jambo ambalo mimi sikuwaamuru walifanye. Mimi nayajua hayo; nimeyashuhudia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu aliniagiza nimwambie hivi Shemaya wa Nehelamu: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Umepeleka barua kwa jina lako kwa wakazi wote wa Yerusalemu na kwa kuhani Sefania mwana wa Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Katika barua hiyo, ulimwambia Sefania hivi: ‘Mwenyezi-Mungu amekufanya wewe Sefania kuwa kuhani badala ya kuhani Yehoyada, uwe mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Ni wajibu wako kumtia gerezani na kumfunga minyororo mwendawazimu yeyote anayetabiri. Kwa nini basi, hukumkemea Yeremia kutoka Anathothi anayekutabiria? Maana yeye alituma taarifa huko Babuloni kwamba uhamisho wenu utakuwa wa muda mrefu, na kusema mjenge nyumba, mkae; mlime mashamba, mpande mbegu na kula mazao yake!’” Kuhani Sefania aliisoma barua hiyo mbele ya nabii Yeremia. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Yeremia: “Wapelekee watu wote walioko uhamishoni ujumbe huu: Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Shemaya wa Nehelamu: Shemaya amewatabirieni, hali mimi sikumtuma, akawafanya muuamini uongo.
Yeremia 29:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli; (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;) kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hata Babeli, kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli), kusema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli; Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake; oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue. Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa BWANA; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha. Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema BWANA. Maana BWANA asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa. Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema BWANA; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka. Maana mmesema, BWANA ametuinulia manabii huko Babeli. Maana BWANA asema hivi, katika habari za mfalme aketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, na katika habari za watu wote wakaao ndani ya mji huu, ndugu zenu wasiokwenda pamoja nanyi kufungwa; BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitaleta juu yao upanga, na njaa, na tauni, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana. Nami nitawafuatia kwa upanga, na njaa, na tauni, nami nitawatoa watupwe huko na huko katika falme zote za dunia, wawe kitu cha kulaaniwa, na cha kushangaza, na cha kuzomewa, na cha kulaumiwa, katika mataifa yote nilikowafukuza. Kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu, asema BWANA, ambayo naliwatuma watumishi wangu, hao manabii, nikiamka mapema, na kuwatuma; lakini hamkutaka kusikiliza, asema BWANA. Basi, lisikieni neno la BWANA, ninyi nyote mliochukuliwa mateka, niliowapeleka toka Yerusalemu mpaka Babeli. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za Ahabu, mwana wa Kolaya, na katika habari za Sedekia, mwana wa Maaseya, wawatabiriao ninyi maneno ya uongo kwa jina langu; Tazama, nitawatia katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu. Tena katika habari zao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, kusema, BWANA akufanye uwe kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni; kwa sababu wametenda upumbavu katika Israeli, nao wamezini na wake za jirani zao, nao wamenena maneno ya uongo kwa jina langu, nisiyowaamuru; nami ndimi nijuaye, nami ni shahidi, asema BWANA. Na katika habari za Shemaya, Mnehelami, utanena, ukisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Kwa kuwa kwa jina lako mwenyewe umewapelekea barua watu wote walioko Yerusalemu, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, na makuhani wote, kusema, BWANA amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya BWANA, kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na pingu. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu, ambaye ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake. Na Sefania, kuhani, akasoma barua hii masikioni mwa Yeremia nabii. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema, Uwapelekee habari watu wote waliohamishwa, kusema, BWANA asema hivi, katika habari za Shemaya, Mnehelami; Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, lakini sikumtuma mimi, naye amewatumainisha neno la uongo
Yeremia 29:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno haya ndiyo maneno ya barua, ambayo nabii Yeremia alituma toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadneza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hadi Babeli; (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;) kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hadi Babeli, kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli), kusema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli; Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake; oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue. Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa BWANA; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha. Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema BWANA. Maana BWANA asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa. Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za baadaye. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema BWANA; nami nitawaleta tena, hadi mahali ambapo kutoka hapo niliwafanya mchukuliwe mateka. Maana mmesema, BWANA ametuinulia manabii huko Babeli. Maana BWANA asema hivi, kuhusu mfalme aketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, na kuhusu watu wote wakaao ndani ya mji huu, ndugu zenu wasiokwenda pamoja nanyi kufungwa; BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitaleta juu yao upanga, na njaa, na tauni, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana. Nami nitawafuatia kwa upanga, na njaa, na tauni, nami nitawatoa watupwe huku na huko katika falme zote za dunia, wawe kitu cha kulaaniwa, na cha kushangaza, na cha kuzomewa, na cha kulaumiwa, katika mataifa yote nilikowafukuza. Kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu, asema BWANA, ambayo niliwatuma watumishi wangu, hao manabii, nikiamka mapema, na kuwatuma; lakini hamkutaka kusikiliza, asema BWANA. Basi, lisikieni neno la BWANA, ninyi nyote mliochukuliwa mateka, niliowafukuza toka Yerusalemu mpaka Babeli. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, kuhusu Ahabu, mwana wa Kolaya, na kuhusu Sedekia, mwana wa Maaseya, wanaowatabiria ninyi maneno ya uongo kwa jina langu; Tazama, nitawatia katika mikono ya Nebukadneza, mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu. Tena kwa ajili yao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, kusema, BWANA akufanye uwe kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni; kwa sababu wametenda upumbavu katika Israeli, nao wamezini na wake za jirani zao, nao wamenena maneno ya uongo kwa jina langu, nisiyowaamuru; nami ndimi nijuaye, nami ni shahidi, asema BWANA. Na kuhusu Shemaya, Mnehelami, utanena, ukisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Kwa kuwa kwa jina lako mwenyewe umewapelekea barua watu wote walioko Yerusalemu, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, na makuhani wote, kusema, BWANA amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya BWANA, kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na pingu. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu, ambaye ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake. Na Sefania, kuhani, akasoma barua hii masikioni mwa Yeremia nabii. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema, Uwapelekee habari watu wote waliohamishwa, kusema, BWANA asema hivi, kuhusu Shemaya, Mnehelami; Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, lakini sikumtuma mimi, naye amewatumainisha neno la uongo
Yeremia 29:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu. (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.) Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema: Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake. Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake, nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue. Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni BWANA kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.” Naam, hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema BWANA, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nitaonekana kwenu,” asema BWANA, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema BWANA. Mnaweza mkasema, “BWANA ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,” lakini hili ndilo asemalo BWANA kuhusu mfalme aketiaye kiti cha enzi cha Daudi, na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, ndugu zenu ambao hawakwenda pamoja nanyi uhamishoni. Naam, hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao, nami nitawafanya kuwa kama tini dhaifu zile ambazo ni mbovu sana zisizofaa kuliwa. Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni, nami nitawafanya kitu cha kuchukiza sana kwa falme zote za dunia, na kuwa kitu cha laana na cha kuogofya, cha dharau na kukemewa, miongoni mwa mataifa yote nitakakowafukuzia. Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema BWANA, “maneno ambayo niliwatumia tena na tena kupitia watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema BWANA. Kwa hiyo, sikieni neno la BWANA, enyi nyote mlio uhamishoni, niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu. Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya, na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa. Kwa ajili yao, watu wote wa uhamisho kutoka Yuda walioko Babeli watatumia laana hii: ‘BWANA na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma kwa moto.’ Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya. Nami nayajua haya, na ni shahidi wa jambo hilo,” asema BWANA. Mwambie Shemaya Mnehelami, “Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania, ‘BWANA amekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada ili uwe msimamizi wa nyumba ya BWANA. Unapaswa kufunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu yeyote anayejifanya nabii. Kwa nini basi hukumkemea Yeremia Mwanathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu? Ametutumia ujumbe huu huku Babeli: Mtakuwako huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae; pandeni mashamba na mle mazao yake.’ ” Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: “Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni: ‘Hili ndilo BWANA asemalo kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo