Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 11:1-17

Yeremia 11:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; “Sikiliza masharti ya agano hili, kisha nenda ukawatangazie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu. Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Na alaaniwe mtu yeyote asiyejali masharti ya agano hili. Hili ni agano nililowapa wazee wenu nilipowatoa nchini Misri, kutoka katika tanuri la chuma. Niliwaambia wanitii na kufanya yote niliyowaamuru, na kwamba wakifanya hivyo, watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Wakifuata masharti hayo, mimi nitatimiza ahadi niliyowapa wazee wenu, kwamba nitawapa nchi inayotiririka maziwa na asali, kama ilivyo hadi leo.” Nami nikajibu: “Na iwe hivyo, ee Mwenyezi-Mungu.” Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Tangaza masharti hayo yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Waambie watu wayasikilize masharti ya agano hili na wayatekeleze. Maana niliwaonya vikali wazee wao nilipowatoa katika nchi ya Misri, na nimeendelea kuwaonya wanitii mpaka siku hii ya leo. Lakini wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza. Badala yake, kila mmoja wao alizidi kuwa mkaidi na mwovu. Basi, niliwaadhibu kulingana na masharti ya agano hili nililowaamuru walishike, lakini hao wakakataa kulishika.” Tena Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wanafanya njama za kuniasi. Wameurudia uovu wa wazee wao ambao walikataa kusikiliza maneno yangu; wameiabudu miungu mingine na kuitumikia. Watu wa Israeli na watu wa Yuda wamevunja agano nililofanya na wazee wao. Kwa hiyo, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu ninawaonya kwamba nitawaletea maafa ambayo hawataweza kuepukana nayo. Hata kama wakinililia namna gani, sitawasikiliza. Hapo ndipo watu wa Israeli na Yerusalemu watakapoiendea miungu yao ambayo wanaifukizia ubani. Lakini miungu hiyo haitaweza kuwaokoa wakati huo wa taabu zao. Miungu yako, ewe Yuda imekuwa mingi kama ilivyo miji yako; kama zilivyo nyingi barabara za Yerusalemu, ndivyo zilivyo nyingi madhabahu walizomjengea mungu kinyaa Baali, ili kumfukizia ubani. Basi, wewe Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, wala usiwaombee dua. Maana, hata wakiniomba wanapotaabika, mimi sitawasikiliza.” Mwenyezi-Mungu asema: “Watu niwapendao wana haki gani kuingia hekaluni mwangu wakati wametenda maovu? Je, wanadhani nadhiri na nyama zilizowekwa wakfu zitawaondolea maafa? Je, hayo yatawafurahisha? Wakati fulani, mimi nilisema, wao ni mzeituni wenye majani mabichi, mzeituni mzuri na wenye matunda mema; lakini sasa, kwa ngurumo ya dhoruba kubwa, nitauchoma moto na kuyateketeza matawi yake. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi niliuotesha huu mzeituni; lakini natangaza maafa dhidi yake kwa sababu ya maovu ambayo watu wa Israeli na Yuda wameyafanya. Wamenikasirisha kwa kumfukizia ubani mungu Baali.”

Shirikisha
Soma Yeremia 11

Yeremia 11:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; ukawaambie, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya, Niliyowaamuru baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika tanuri ya chuma, nikisema, Itiini sauti yangu, mkafanye sawasawa na yote niwaagizayo ninyi; ndivyo mtakavyokuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu; ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi itiririkayo maziwa na asali, kama ilivyo hivi leo. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee BWANA. Naye BWANA akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye. Kwa maana niliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu. Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya. Naye BWANA akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu. Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, lakini sitawasikiliza. Ndipo miji ya Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, watakwenda na kuwalilia miungu wawafukiziao uvumba; lakini hawatawaokoa hata kidogo wakati wa taabu yao. Maana hesabu ya miungu yako, Ee Yuda, ni sawasawa na hesabu ya miji yako; na kama ilivyo hesabu ya njia za Yerusalemu, ndivyo mlivyosimamisha madhabahu za kitu kile cha aibu, madhabahu za kumfukizia Baali uvumba. Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao. Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha. BWANA alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika. Kwa maana BWANA wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba.

Shirikisha
Soma Yeremia 11

Yeremia 11:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; ukawaambie, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya, niliyowaamuru baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika tanuru ya chuma, nikisema, Itiini sauti yangu, mkafanye sawasawa na yote niwaagizayo ninyi; ndivyo mtakavyokuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu; ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi ijaayo maziwa na asali, kama ilivyo leo hivi. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee BWANA. Naye BWANA akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye. Kwa maana naliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu. Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya. Naye BWANA akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu. Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, walakini sitawasikiliza. Ndipo miji ya Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, watakwenda na kuwalilia miungu wawafukiziao uvumba; lakini hawatawaokoa hata kidogo wakati wa taabu yao. Maana hesabu ya miungu yako, Ee Yuda, ni sawasawa na hesabu ya miji yako; na kama ilivyo hesabu ya njia za Yerusalemu, ndivyo mlivyosimamisha madhabahu za kitu kile cha aibu, madhabahu za kumfukizia Baali uvumba. Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao. Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha. BWANA alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika. Kwa maana BWANA wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba.

Shirikisha
Soma Yeremia 11

Yeremia 11:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA: “Sikia maneno ya agano hili, nawe uwaambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu. Waambie kwamba hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Amelaaniwa mtu ambaye hatayatii maneno ya agano hili, maneno niliyowaamuru baba zenu nilipowatoa katika nchi ya Misri, kutoka tanuru la kuyeyushia vyuma.’ Nilisema, ‘Nitiini mimi na mfanye kila kitu ninachowaamuru, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Kisha nitatimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi itiririkayo maziwa na asali,’ nchi ambayo mnaimiliki leo.” Nikajibu, “Amen, BWANA.” BWANA akaniambia, “Tangaza maneno haya yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu: ‘Sikilizeni maneno ya agano hili na kuyafuata. Tangu wakati ule niliwapandisha baba zenu kutoka Misri mpaka leo, niliwaonya tena na tena, nikisema “Nitiini mimi.” Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Hivyo nikaleta juu yao laana zote za agano nililokuwa nimewaamuru wao kulifuata, lakini wao hawakulishika.’ ” Kisha BWANA akaniambia, “Kuna shauri baya linaloendelea miongoni mwa watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu. Wamerudia dhambi za baba zao, waliokataa kusikiliza maneno yangu. Wameifuata miungu mingine kuitumikia. Nyumba zote mbili za Israeli na Yuda zimelivunja agano nililofanya na baba zao. Kwa hivyo, hili ndilo asemalo BWANA: ‘Nitaleta juu yao maafa ambayo hawawezi kuyakimbia. Hata kama wakinililia, sitawasikiliza. Miji ya Yuda na watu wa Yerusalemu watakwenda kuililia miungu ambayo wameifukizia uvumba, lakini haitawasaidia kamwe wakati maafa yatakapowapiga. Mnayo miungu mingi kama miji mliyo nayo, ee Yuda, nazo madhabahu mlizozijenga za kufukizia uvumba huyo mungu wa aibu Baali ni nyingi kama barabara za Yerusalemu.’ “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yoyote au kunisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao. “Mpenzi wangu anafanya nini hekaluni mwangu, anapofanya mashauri yake maovu na wengi? Je, nyama iliyowekwa wakfu yaweza kuondolea mbali adhabu yako? Unapojiingiza katika ubaya wako, ndipo unashangilia.” BWANA alikuita mti wa mzeituni uliostawi ulio na matunda mazuri kwa sura. Lakini kwa ngurumo ya mawimbi makuu atautia moto, nayo matawi yake yatavunjika. BWANA Mwenye Nguvu Zote, aliyekupanda, ametamka maafa kwa ajili yako, kwa sababu nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda mmefanya maovu na kunikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba.

Shirikisha
Soma Yeremia 11

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha