Waamuzi 9:50-57
Waamuzi 9:50-57 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka. Lakini kulikuwa na mnara imara katikati ya mji. Basi, wakazi wote wa mji huo wanaume na wanawake wakakimbilia humo na kujifungia ndani. Wakapanda kwenye paa la mnara huo. Abimeleki aliufikia mnara na kuushambulia, kisha, aliukaribia mlango wa mnara autie moto. Naye mwanamke mmoja akatupa jiwe la juu la kusagia, akamponda Abimeleki kichwa. Kisha Abimeleki akamwita haraka kijana wake aliyembebea silaha akamwambia, “Chukua upanga wako uniue, wasije watu wakasema kuwa niliuawa na mwanamke.” Kijana akachukua upanga wake, akamchoma na kumuua. Waisraeli walipoona kwamba Abimeleki amekufa, wakaondoka na kurudi kila mmoja nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyomwadhibu Abimeleki kwa kosa lake dhidi ya baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Vilevile Mungu aliwafanya watu wa Shekemu waadhibiwe kwa uovu wao walioufanya. Hivyo, laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawapata.
Waamuzi 9:50-57 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji. Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini; uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.
Waamuzi 9:50-57 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka. Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara. Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto, mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake. Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa. Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.
Waamuzi 9:50-57 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akauzingira na kuutwaa. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na mnara wenye nguvu, na watu wote wanaume na wanawake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la mnara. Abimeleki akauendea huo mnara na kupigana nao; naye akaukaribia mlango wa mnara ili auteketeze. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu, Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. Kwa hiyo, Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, kwa kuwaua hao nduguze watu sabini; uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajia juu yao.