Waamuzi 4:8-16
Waamuzi 4:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Baraki akamwambia Debora, “Kama utakwenda pamoja nami, nitakwenda. Lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.” Debora akamjibu, “Sawa. Nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata heshima yoyote ya ushindi, maana Mwenyezi-Mungu, atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Basi, Debora akafuatana na Baraki kwenda Kedeshi. Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye. Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi. Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori, alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni. Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000. Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. Baraki akalifuatia jeshi hilo na magari mpaka Harosheth-hagoimu na kuwaua wanajeshi wote wa Sisera kwa mapanga; hakubaki hata mtu mmoja.
Waamuzi 4:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana BWANA atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi. Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye. Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saananimu, karibu na Kedeshi. Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori. Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia tisa, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni. Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo BWANA amemtia Sisera katika mkono wako. Je! BWANA hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata. BWANA akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hadi Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja.
Waamuzi 4:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana BWANA atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi. Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye. Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi. Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori. Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia kenda, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni. Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo BWANA amemtia Sisera katika mkono wako. Je! BWANA hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata. BWANA akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hata Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja.
Waamuzi 4:8-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitakwenda, lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.” Debora akamwambia, “Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwa BWANA atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi, mahali ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu 10,000 wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda pamoja naye. Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wengine, yaani, wazao wa Hobabu, mkwewe Mose, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulioko Saananimu, karibu na Kedeshi. Sisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori, Sisera akakusanya pamoja magari yake yote 600 ya chuma na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu mpaka Mto wa Kishoni. Ndipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayo BWANA amemtia Sisera mikononi mwako. Je, BWANA hakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu 10,000. BWANA akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake na kukimbia kwa miguu. Lakini Baraka akafuata magari pamoja na jeshi mpaka Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.