Waamuzi 11:1-33
Waamuzi 11:1-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Huko Gileadi kulikuwa na mpiganaji hodari aitwaye Yeftha, mwana wa mama mmoja malaya, na baba yake aliitwa Gileadi. Gileadi alikuwa pia na wana wengine kwa mke wake wa halali. Watoto wa mke huyo walipokuwa wakubwa, walimfukuza Yeftha kutoka nyumbani, wakamwambia, “Wewe huna haki ya kupata urithi kutoka kwa baba yetu, maana wewe ni mtoto wa mwanamke mwingine.” Basi, Yeftha akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu. Huko watu ovyo wakakusanyika kujiunga naye, wakamfuata katika safari zake za mashambulio. Baada ya muda fulani, Waamoni waliwashambulia Waisraeli. Wakati vita vilipopamba moto, wazee wa Gileadi wakaenda kumleta Yeftha kutoka nchi ya Tobu, wakamwambia, “Njoo utuongoze katika vita vyetu na Waamoni.” Lakini Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Je, si mlinichukia hata mkanifukuza kutoka kwa jamaa ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa mkiwa katika taabu?” Hao wazee wa Gileadi wakamwambia “Ndio maana tumekujia ili uende nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu na wa wakazi wote wa Gileadi.” Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Kama mkinirudisha nyumbani kupigana na Waamoni halafu Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu, mimi nitakuwa kiongozi wenu.” Wale wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu. Hakika tutafanya kama ulivyosema.” Yeftha akafuatana na wazee wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi wao. Yeftha akasema masharti yake huko Mizpa mbele ya Mwenyezi-Mungu Yeftha akapeleka ujumbe kwa mfalme wa Amoni akamwambia, “Una ugomvi gani nasi hata uje kuishambulia nchi yetu?” Mfalme wa Amoni akawajibu hao wajumbe, “Waisraeli walipotoka Misri, walichukua nchi yangu kutoka mto Arnoni hadi mto Yaboki na mto Yordani. Sasa nirudishie nchi hiyo kwa amani.” Yeftha akatuma tena wajumbe kwa mfalme wa Amoni wamwambie kwa niaba yake, “Waisraeli hawakuchukua nchi ya Wamoabu wala nchi ya Waamoni. Lakini Waisraeli walipotoka Misri, walisafiri jangwani hadi bahari ya Shamu mpaka Kadeshi. Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu wakimwomba awaruhusu kupita katika nchi yake, lakini mfalme wa Edomu akakataa. Basi wakamwomba ruhusa mfalme wa Moabu naye pia akakataa. Kwa hiyo Waisraeli wakabaki Kadeshi. Kisha wakasafiri wakipitia jangwani kuzunguka nchi ya Edomu na Moabu mpaka walipofika upande wa mashariki wa Moabu, wakapiga kambi ngambo ya mto Arnoni. Lakini hawakuingia eneo la Moabu. Mto Arnoni ndio uliokuwa mpaka wa Moabu. Hapo Waisraeli walituma wajumbe kwa mfalme Sihoni wa Waamori huko Heshboni wakamwomba awaruhusu kupita katika nchi yake waende katika nchi yao. Lakini Sihoni hakuwakubali Waisraeli wapite katika nchi yake. Basi, Sihoni akakusanya watu wake wote, akapiga kambi huko Yahasa, akawashambulia Waisraeli. Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni pamoja na watu wake mikononi mwa Waisraeli, wakawashinda. Hivyo Waisraeli wakachukua nchi yote ya Waamori ambao walikuwa wanaishi huko. Walilichukua eneo lote la Waamori tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki na tangu jangwani upande wa mashariki hadi mto Yordani magharibi. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akawafukuza Waamori mbele ya Waisraeli. Je, wewe unataka kutunyanganya nchi yetu? Tosheka na kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa. Lakini nchi yoyote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, amewafukuza wakazi wake, akatupa sisi, hiyo ni mali yetu sisi. Je, unadhani wewe una nguvu kuliko Balaki mwana wa Zipora aliyekuwa mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli au kupigana nao. Wakati wote Waisraeli walipoishi mjini Heshboni na vijiji vyake, na mji wa Aroeri na vijiji vyake pamoja na miji yote iliyo ukingoni mwa mto Arnoni kwa muda wa miaka 300, kwa nini hukulikomboa eneo hilo wakati huo? Mimi sijakukosea kitu na ndio maana unafanya kosa unaponishambulia. Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mwamuzi ataamua leo hii kati ya Waisraeli na watu wa Amoni.” Lakini mfalme wa Amoni alipuuza ujumbe huo wa Yeftha. Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Yeftha, naye akaondoka na kupitia Gileadi na Manase, akarudi Mizpa katika nchi ya Gileadi na kuendelea hadi Amoni. Yeftha akamwapia Mwenyezi-Mungu akisema, “Kama utawatia Waamoni mikononi mwangu, basi, yeyote atakayetoka nje kutoka nyumbani mwangu kuja kunilaki nitakapokuwa narudi baada ya kuwashinda Waamoni, huyo atakuwa wako wewe Mwenyezi-Mungu. Huyo nitakutolea sadaka ya kuteketezwa.” Basi, Yeftha akavuka mto, akapigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia Waamoni mikononi mwake. Akajipatia ushindi mkubwa, akateka maeneo ishirini yaliyokuwa kati ya Aroeri, sehemu zilizozunguka Minithi na Abel-keramimu. Basi Waamoni wakashindwa kabisa na Waisraeli.
Waamuzi 11:1-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya baba yetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; nao watu mabaradhuli walikwenda na kushirikiana na Yeftha katika uvamizi wake, wakatoka kwenda pamoja naye. Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini basi mnanijia hivi sasa wakati mkiwa katika taabu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, “Kama mkinirejesha kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye BWANA akawatoa mbele yangu, je! Nitakuwa kiongozi wenu?” Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye BWANA atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kiongozi, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya BWANA huko Mispa. Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijia kupigana juu ya nchi yangu? Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha, “Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea wakitoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena kwa amani.” Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni; akamwambia, Yeftha anakuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni; lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walipitia katika jangwa hadi Bahari ya Shamu, na Kadeshi; ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hangewasikiliza. Pia waliwatuma wajumbe kwa mfalme wa Moabu; wala naye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi. Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki mwa nchi ya Moabu, wakapiga kambi upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu. Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Tunakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu. Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapiga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli. BWANA, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, waliokaa katika nchi hiyo. Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hilo jangwa hadi Yordani. Basi sasa yeye BWANA, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe unataka kuchukua mahali pao? Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika si sisi ndio watu wa kutamalaki vyote ambavyo BWANA, Mungu wetu ametwaa kwa manufaa yetu? Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lolote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao? Wakati Israeli walipokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona hamkuikomboa wakati huo? Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye BWANA, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni. Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuusikiza ujumbe aliotumiwa na Yeftha. Ndipo Roho ya BWANA ikamjia Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni. Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Ikiwa utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na ushindi kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye BWANA akawaua mkononi mwake. Akawapiga kutoka Aroeri hadi kufikia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa pigo kuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.
Waamuzi 11:1-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye. Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye BWANA akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye BWANA atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya BWANA huko Mispa. Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu? Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata. Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni; akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni; lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi; ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi. Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu. Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu. Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli. BWANA, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo. Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani. Basi sasa yeye BWANA, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki? Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye BWANA, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki. Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao? Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo? Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye BWANA, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni. Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea. Ndipo roho ya BWANA ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni. Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye BWANA akawaua mkononi mwake. Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.
Waamuzi 11:1-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Yefta Mgileadi alikuwa mtu shujaa. Baba yake alikuwa Gileadi, naye mama yake alikuwa kahaba. Mke wa Gileadi akamzalia wana wengine, nao watoto hao walipokua, wakamfukuza Yefta na kumwambia, “Wewe huwezi kupata urithi katika jamii yetu, kwa sababu wewe ni mwana wa mwanamke mwingine.” Basi Yefta akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu, mahali ambako watu waasi walijiunga naye na kumfuata. Baada ya muda Waamoni wakafanya vita na Israeli, viongozi wa Gileadi wakaenda kumchukua Yefta katika nchi ya Tobu. Wakamwambia Yefta, “Uwe jemadari wetu, ili tuweze kupigana na Waamoni.” Yefta akawaambia, “Je, hamkunichukia mimi na kunifukuza katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa, wakati mna matatizo.” Viongozi wa Gileadi wakamwambia Yefta, “Lakini sasa tumegeuka kukuelekea wewe, ili uende pamoja nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu juu ya watu wote wa Gileadi.” Yefta akawaambia, “Ikiwa mtanirudisha kwetu kupigana na Waamoni, naye BWANA akanisaidia kuwashinda, Je, ni kweli nitakuwa kiongozi wenu?” Viongozi wa Gileadi wakamjibu Yefta, “BWANA ndiye shahidi yetu. Kwa hakika tutafanya kama usemavyo.” Basi Yefta akaenda na viongozi wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi na jemadari wao. Naye akarudia maneno yake yote mbele za BWANA huko Mispa. Ndipo Yefta akatuma wajumbe kwa mfalme wa Waamoni akisema, “Una nini juu yetu, hata umekuja kushambulia nchi yetu?” Mfalme wa Waamoni akawajibu wajumbe wale wa Yefta, “Wakati Waisraeli walipopanda kutoka Misri, waliichukua nchi yangu kuanzia Arnoni mpaka Yaboki, hadi kufikia Yordani. Sasa rudisha kwa amani.” Yefta akarudisha wajumbe kwa mfalme wa Waamoni, kusema: “Hili ndilo asemalo Yefta, Israeli hawakuchukua nchi ya Moabu wala ya Waamoni. Lakini walipopanda kutoka Misri, Israeli walipitia katika jangwa hadi Bahari ya Shamu na wakafika Kadeshi. Ndipo Israeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu, wakisema, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako,’ Lakini mfalme wa Edomu hakutusikia. Wakapeleka pia wajumbe kwa mfalme wa Moabu, naye akakataa. Kwa hiyo Israeli wakakaa huko Kadeshi. “Baadaye wakasafiri kupitia jangwa, wakiambaa na nchi za Edomu na Moabu, wakapitia upande wa mashariki wa nchi ya Moabu na kupiga kambi upande mwingine wa Arnoni. Hawakuingia katika nchi ya Moabu, kwa kuwa Arnoni ilikuwa mpaka wake. “Kisha Israeli wakatuma wajumbe kwa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, na kumwambia, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako ili kufikia mahali petu.’ Hata hivyo, Sihoni hakuwaamini Waisraeli kupita katika nchi yake. Akaandaa jeshi lake lote na kupiga kambi huko Yahasa, nao wakapigana na Israeli. “Ndipo BWANA, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawashinda. Israeli wakaitwaa nchi yote ya Waamori, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo, wakiiteka nchi yote kuanzia Arnoni mpaka Yaboki, na kutoka jangwani mpaka Yordani. “Basi kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, amewafukuza Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, wewe unayo haki gani ya kuitamalaki? Je, haikupasi kuchukua kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa? Vivyo hivyo, chochote kile BWANA Mungu wetu alichotupa sisi, tutakimiliki. Je, wewe ni bora kuliko Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Je, yeye alishagombana na Israeli au kupigana nao wakati wowote? Kwa maana kwa miaka 300 Israeli wameishi Heshboni na vijiji vyake, Aroeri na vijiji vyake, na katika miji yote iliyo kando ya Arnoni. Kwa nini wewe haukuyachukua wakati huo? Mimi sijakukosea jambo lolote, bali wewe ndiye unayenikosea kwa kufanya vita nami. Basi BWANA, aliye Mwamuzi, leo na aamue ugomvi kati ya Waisraeli na Waamoni.” Hata hivyo, Mfalme wa Waamoni, hakuyajali maneno ya ujumbe wa Yefta. Ndipo Roho wa BWANA akaja juu ya Yefta. Akapita katikati ya Gileadi na Manase, pia akapita katika Mispa ya Gileadi, na kutokea huko akasonga mbele kushambulia Waamoni. Naye Yefta akaweka nadhiri mbele za BWANA akisema, “Ikiwa utawatia Waamoni mikononi mwangu, chochote kile kitakachotoka katika mlango wa nyumba yangu cha kwanza ili kunilaki nirudipo kwa amani katika kuwashinda Waamoni, kitakuwa ni cha BWANA na nitakitoa kuwa sadaka ya kuteketezwa.” Ndipo Yefta akavuka kupigana na hao Waamoni, naye BWANA akawatia mkononi mwake. Akawapiga kwa ushindi mkubwa kuanzia Aroeri mpaka karibu na Minithi na kuendelea mpaka Abel-Keramimu, miji yote iliyopigwa ni ishirini. Basi Israeli wakawashinda Waamoni.