Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 1:5-30

Waamuzi 1:5-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mji huo walimkuta mfalme Adoni-bezeki, wakapigana naye na kuwashinda Wakanaani na Waperizi. Adoni-bezeki akakimbia, lakini walimfuatia, wakamkamata, wakamkata vidole gumba vya mikono na miguu. Adoni-bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokatwa vidole gumba vya mikono na miguu waliokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa kama nilivyotenda.” Wakampeleka Yerusalemu, akafia huko. Watu wa kabila la Yuda waliushambulia mji wa Yerusalemu na kuuteka. Waliwaua wakazi wake kwa mapanga na kuuteketeza mji kwa moto. Baadaye, watu wa kabila la Yuda walikwenda kupigana na Wakanaani walioishi kwenye nchi ya milima, Negebu na kwenye nchi tambarare. Waliwashambulia pia Wakanaani walioishi katika mji wa Hebroni ambao hapo awali uliitwa Kiriath-arba, wakashinda makabila ya Sheshai, Himani na Talmai. Kutoka huko watu wa kabila la Yuda walikwenda kuushambulia mji wa Debiri; ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. Kalebu akatangaza: “Mtu yeyote atakayefaulu kuuteka mji wa Kiriath-seferi, nitamwoza binti yangu Aksa.” Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi na mdogo wake Kalebu, akauteka, naye Kalebu akamtoa bintiye Aksa aolewe na Othnieli. Aksa alipowasili kwa Othnieli, akamwambia Othnieli amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa alikuwa amepanda punda na aliposhuka chini baba yake alimwuliza, “Ungependa nikupe nini?” Akamjibu, “Nipe zawadi! Naomba unipe chemchemi za maji kwani eneo ulilonipa huko Negebu ni kavu.” Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini. Wazawa wa Keni ambaye alikuwa baba mkwe wa Mose, walifuatana na watu wa kabila la Yuda kutoka Mji wa Mitende yaani mji wa Yeriko, mpaka jangwa la Yuda karibu na Aradi, wakafanya makao yao huko pamoja na watu wa Yuda. Watu wa kabila la Yuda walishirikiana na ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, wakawashinda Wakanaani waliokaa Sefathi. Waliuangamiza kabisa mji huo na kugeuza jina lake kuwa Horma. Watu wa kabila la Yuda pia waliteka miji ya Gaza na eneo lake, Ashkeloni na eneo lake, na Ekroni na eneo lake. Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na watu wa kabila la Yuda, nao wakaiteka nchi ya milima. Lakini hawakuweza kuwashinda wenyeji wa nchi tambarare kwa sababu magari yao ya vita yalikuwa ya chuma. Mji wa Hebroni ukakabidhiwa kwa Kalebu kufuatana na maagizo ya Mose. Kalebu akazifukuza kutoka huko koo tatu za Anaki. Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mjini Yerusalemu; ndiyo maana Wayebusi wanakaa pamoja na watu wa kabila la Benyamini mjini Yerusalemu mpaka leo. Watu wa makabila ya Yosefu waliushambulia mji wa Betheli, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja nao. Kwanza walikuwa wamewatuma wapelelezi kwenda kuupeleleza mji wa Betheli. Mji huo hapo awali uliitwa Luzu. Wapelelezi hao walimwona mtu mmoja akitoka mjini, wakamwambia, “Tafadhali, tuoneshe njia inayoingia mjini, nasi tutakutendea kwa wema.” Akawaonesha njia ya kuingia mjini. Basi, wakaingia na kuangamiza kila mtu aliyekuwamo. Lakini wakamwacha salama mtu huyo na jamaa yake. Mtu huyo akahamia nchi ya Wahiti, huko akajenga mji ambao aliuita Luzu; na mji huo unaitwa hivyo mpaka leo. Watu wa kabila la Manase hawakuwafukuza wakazi wa miji ya Beth-sheani na vijiji vyake, Taanaki na vijiji vyake, Dori na vijiji vyake, Ibleamu na vijiji vyake, na Megido pamoja na vijiji vyake. Wakanaani waliendelea kukaa huko. Hata Waisraeli walipokuwa na nguvu hawakuwafukuza Wakanaani bali waliwapa kazi za kulazimishwa. Watu wa kabila la Efraimu hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Gezeri, na hawa waliishi huko pamoja na watu wa Efraimu. Watu wa kabila la Zebuluni hawakuwafukuza wakazi wa mji wa Kitroni, wala wale wa mji wa Nahalali, waliendelea kukaa pamoja nao wakiwafanyiza kazi za kulazimishwa.

Shirikisha
Soma Waamuzi 1

Waamuzi 1:5-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi. Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandama na kumshika, wakamkata vidole vyake vya gumba vya mikono na vya miguu. Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vidole vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo hivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko. Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji. Baadaye wana wa Yuda wakateremka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi yenye milima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela. Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai. Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.) Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe. Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa. Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo? Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini. Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao. Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma. Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake. BWANA alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi yenye milima; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma. Kisha wakampa huyo Kalebu Hebroni, kama alivyonena Musa naye akawafukuza wale wana watatu wa Anaki. Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mji wa Yerusalemu; bali Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Benyamini ndani ya Yerusalemu hata hivi leo. Nyumba ya Yusufu nayo, wao nao walikwea kwenda juu ya Betheli; naye BWANA alikuwa pamoja nao. Kisha watu wa ukoo wa Yusufu wakatuma watu waende kuupeleleza Betheli. (Jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Luzu.) Hao wapelelezi walimwona mtu atoka katika huo mji, wakamwambia, Tafadhali, utuoneshe njia ya kuingia mji huu, nasi tutakutendea mema. Basi akawaonesha njia ya kuingia mji, nao wakaupiga huo mji kwa makali ya upanga; lakini huyo mtu walimwacha aende zake, na watu wote wa jamaa yake. Huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akaliita jina la huo mji Luzu; nalo ndilo jina lake hata hivi leo. Tena Manase hakuwatoa wenyeji wa Beth-sheani na miji yake, wala hao waliokaa Taanaki na miji yake, wala hao waliokaa Dori na miji yake, wala hao waliokaa Ibleamu na miji yake, wala hao waliokaa Megido na miji yake; lakini hao Wakanaani walikuwa hawakukubali kuiacha nchi hiyo. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepata nguvu, ndipo walipowatia hao Wakanaani katika kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa. Efraimu naye hakuwatoa Wakanaani waliokuwa wakikaa katika Gezeri; lakini Wakanaani walikaa ndani ya Gezeri kati yao. Zabuloni naye hakuwatoa wenyeji wa Kitroni, wala hao waliokaa katika Nahalali; lakini Wakanaani walikaa kati yao, wakalazimishwa shokoa.

Shirikisha
Soma Waamuzi 1

Waamuzi 1:5-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi. Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu. Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko. Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji. Baadaye wana wa Yuda wakatelemka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi ya milimani, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela. Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai. Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.) Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe. Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa. Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo? Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini. Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao. Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma. Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake. BWANA alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma. Kisha wakampa huyo Kalebu Hebroni, kama alivyonena Musa naye akawafukuza wale wana watatu wa Anaki. Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mji wa Yerusalemu; bali Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Benyamini ndani ya Yerusalemu hata hivi leo. Nyumba ya Yusufu nayo, wao nao walikwea kwenda juu ya Betheli; naye BWANA alikuwa pamoja nao. Kisha mbari ya Yusufu wakatuma watu waende kuupeleleza Betheli. (Jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Luzu.) Hao wapelelezi walimwona mtu atoka katika huo mji, wakamwambia, Tafadhali, utuonyeshe maingilio ya mji huu, nasi tutakutendea mema. Basi akawaonyesha maingilio ya mji, nao wakaupiga huo mji kwa makali ya upanga; lakini huyo mtu walimwacha aende zake, na watu wote wa jamaa yake. Huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akaliita jina la huo mji Luzu; nalo ndilo jina lake hata hivi leo. Tena Manase hakuwatoa wenyeji wa Bethsheani na miji yake, wala hao waliokaa Taanaki na miji yake, wala hao waliokaa Dori na miji yake, wala hao waliokaa Ibleamu na miji yake, wala hao waliokaa Megido na miji yake; lakini hao Wakanaani walikuwa hawakukubali kuiacha nchi hiyo. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepata nguvu, ndipo walipowatia hao Wakanaani katika kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa. Efraimu naye hakuwatoa Wakanaani waliokuwa wakikaa katika Gezeri; lakini Wakanaani walikaa ndani ya Gezeri kati yao. Zabuloni naye hakuwatoa wenyeji wa Kitroni, wala hao waliokaa katika Nahalali; lakini Wakanaani walikaa kati yao, wakalazimishwa shokoa.

Shirikisha
Soma Waamuzi 1

Waamuzi 1:5-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafanya Wakanaani na Waperizi wakimbie. Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu. Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Nimewatendea wafalme sabini kama nilivyotendewa na kuwalisha makombo ya chakula chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya, kama yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko. Watu wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto. Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi. Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai. Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambao hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.) Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye. Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?” Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini. Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Mose, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende, wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa ya Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi. Basi watu wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao kushambulia Wakanaani waishio Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka. BWANA alikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya chuma. Kama vile Mose alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki. Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini. Basi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, naye BWANA alikuwa pamoja nao. Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu), wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.” Hivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote. Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo. Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile. Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa. Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao. Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.

Shirikisha
Soma Waamuzi 1