Yakobo 2:1-6
Yakobo 2:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?
Yakobo 2:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu. Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu? Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani?
Yakobo 2:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,” je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea ufalme aliowaahidia wale wanaompenda. Lakini nyinyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamiza na kuwapeleka mahakamani?
Yakobo 2:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Wewe keti hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Wewe simama pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo maovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?