Isaya 9:8-21
Isaya 9:8-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo, utamwangukia Israeli. Watu wote watajua hili: Efraimu na wakazi wa Samaria, wanaosema kwa kiburi na majivuno ya mioyo, “Matofali yameanguka chini, lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa, mitini imeangushwa, lakini tutapanda mierezi badala yake.” Lakini BWANA amemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao na kuchochea watesi wao. Waashuru kutoka upande wa mashariki na Wafilisti kutoka upande wa magharibi wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga, wala hawajamtafuta BWANA Mwenye Nguvu Zote. Kwa hiyo BWANA atakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia, tawi la mtende na tete katika siku moja. Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa, nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia. Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha, nao wale wanaoongozwa wamepotoka. Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana, wala hatawahurumia yatima na wajane, kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu, na kila kinywa kinanena upotovu. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. Hakika uovu huwaka kama moto; huteketeza michongoma na miiba, huwasha moto vichaka vya msituni, hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi. Kwa hasira ya BWANA Mwenye Nguvu Zote nchi itachomwa kwa moto, nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto. Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake. Upande wa kuume watakuwa wakitafuna, lakini bado wataona njaa; upande wa kushoto watakuwa wakila, lakini hawatashiba. Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya mtoto wake mwenyewe: Manase atamla Efraimu, naye Efraimu atamla Manase; nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda.
Isaya 9:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu ametoa tamko dhidi ya Yakobo nalo litampata Israeli. Watu wote watatambua, ukoo wote wa Efraimu na wakazi wa Samaria. Kwa kiburi na majivuno wanasema: “Kuta za matofali zimeanguka lakini sisi tutazijenga kwa mawe yaliyochongwa! Nyumba za boriti za mikuyu zimeharibiwa lakini mahali pake tutajenga za mierezi.” Basi, Mwenyezi-Mungu atawaletea wapinzani na kuwachochea maadui zao. Waaramu upande wa mashariki, Wafilisti upande wa magharibi, wamepanua vinywa vyao kuimeza Israeli. Hata hivyo, hasira yake haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Ingawa aliwaadhibu watu, hawakumrudia Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi kwa muda wa siku moja tu, Mwenyezi-Mungu atakata katika Israeli vichwa na mikia, tawi la mtende na nyasi: Vichwa ndio wazee na waheshimiwa, mikia ndio manabii wafundishao uongo. Wale wanaoongoza watu hawa wamewapotosha, na hao wanaoongozwa nao wamepotoka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu hawahurumii vijana wao, hana huruma juu ya yatima na wajane wao; kwani hakuna hata mmoja amchaye Mungu, kila mtu husema uongo. Hata hivyo, hasira yake haijatulia, bado ameunyosha mkono wake. Uovu huwaka kama moto uteketezao mbigili na miiba; huwaka kama moto msituni, na kutoa moshi mzito upandao angani juu. Kwa ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi nchi imechomwa moto, na watu ni kama kuni za kuuwasha. Hakuna mtu anayemhurumia ndugu yake; wananyanganya upande mmoja na hawatosheki; wanakula upande mwingine lakini hawashibi. Kila mmoja anamshambulia mwenzake. Manase dhidi ya Efraimu, Efraimu dhidi ya Manase na wote wawili dhidi ya Yuda. Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia, bado ameunyosha mkono wake.
Isaya 9:8-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana alimpelekea Yakobo neno, nalo likamfikia Israeli. Nao watu wote watajua, yaani, Efraimu na yeye akaaye Samaria, wasemao kwa kiburi na kwa kujisifu nafsi zao, Matofali yameanguka, lakini sisi tutajenga kwa mawe yaliyochongwa; mikuyu imekatwa lakini sisi tutaweka mierezi badala yake. Kwa sababu hiyo BWANA atawainua adui wa Resini juu yake, naye atawachochea adui zake; Waashuri upande wa mbele, na Wafilisti upande wa nyuma, nao watamla Israeli kwa kinywa kilicho wazi. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Lakini watu hao hawakumwelekea yeye aliyewapiga, wala kumtafuta BWANA wa majeshi. Kwa sababu hiyo BWANA atakata katika Israeli kichwa na mkia, kuti na nyasi, katika siku moja. Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa, na nabii afundishaye uongo ndiye mkia. Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia. Kwa sababu hiyo Bwana hatawafurahia vijana wao, wala hatawahurumia yatima zao wala wajane wao; maana kila mtu ni mnajisi, dhalimu, na kila ulimi hunena upumbavu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Kwa maana uovu huteketeza kama moto; huila mibigili na miiba, naam, huwaka katika vichaka vya mwitu, nao hupaa juu katika mawingu mazito ya moshi. Kwa sababu ya hasira ya BWANA wa majeshi nchi hii inateketea kabisa; watu hawa nao ni kama kuni zitiwazo motoni; hapana mtu amhurumiaye ndugu yake. Hupokonya upande wa mkono wa kulia, nao huona njaa! Hula upande wa mkono wa kushoto, wala hawashibi! Watakula kila mtu nyama ya mkono wake mwenyewe. Manase anamla Efraimu, naye Efraimu anamla Manase; nao wawili pamoja watakuwa juu ya Yuda. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
Isaya 9:8-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana alimpelekea Yakobo neno, likamfikilia Israeli. Nao watu wote watajua, yaani, Efraimu na yeye akaaye Samaria, wasemao kwa kiburi na kwa kujisifu nafsi zao, Matofali yameanguka, lakini sisi tutajenga kwa mawe yaliyochongwa; mikuyu imekatwa lakini sisi tutaweka mierezi badala yake. Kwa sababu hiyo BWANA atawainua adui wa Resini juu yake, naye atawachochea adui zake; Waashuri upande wa mbele, na Wafilisti upande wa nyuma, nao watamla Israeli kwa kinywa kilicho wazi. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Lakini watu hao hawakumwelekea yeye aliyewapiga, wala kumtafuta BWANA wa majeshi. Kwa sababu hiyo BWANA atakata katika Israeli kichwa na mkia, kuti na nyasi, katika siku moja. Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa, na nabii afundishaye uongo ndiye mkia. Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia. Kwa sababu hiyo Bwana hatawafurahia vijana wao, wala hatawahurumia yatima zao wala wajane wao; maana kila mtu ni mnajisi, dhalimu, na kila ulimi hunena upumbavu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Kwa maana uovu huteketeza kama moto; huila mibigili na miiba, naam, huwaka katika vichaka vya mwitu, nao hupaa juu katika mawingu mazito ya moshi. Kwa sababu ya hasira ya BWANA wa majeshi nchi hii inateketea kabisa; watu hawa nao ni kama kuni zitiwazo motoni; hapana mtu amhurumiaye ndugu yake. Hupokonya upande wa mkono wa kuume, nao huona njaa! Hula upande wa mkono wa kushoto, wala hawashibi! Watakula kila mtu nyama ya mkono wake mwenyewe. Manase anamla Efraimu, naye Efraimu anamla Manase; nao wawili pamoja watakuwa juu ya Yuda. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.