Isaya 9:1-7
Isaya 9:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa. Watu waliotembea gizani wameona mwanga mkubwa. Watu walioishi katika nchi ya giza kuu, sasa mwanga umewaangazia. Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa, umeiongeza furaha yake. Watu wanafurahi mbele yako, wana furaha kama wakati wa mavuno, kama wafurahivyo wanaogawana nyara. Maana nira nzito walizobeba, nira walizokuwa wamefungwa, na fimbo ya wanyapara wao, umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani. Viatu vyote vya washambulizi vitani na mavazi yote yenye madoa ya damu yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto. Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”. Utawala wake utastawi daima, amani ya ufalme wake haitakoma. Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi na kutawala juu ya ufalme wake; ataustawisha na kuuimarisha, kwa haki na uadilifu, tangu sasa na hata milele. Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Isaya 9:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo awali aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyovingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto wa kiume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. Mamlaka ya enzi yake yatakuzwa daima, Na kutakuwa na amani isiyo na mwisho, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
Isaya 9:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
Isaya 9:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata hivyo, hapatakuwepo huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Wakati uliopita aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataiheshimu Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, kando ya Yordani: Watu wanaotembea katika giza wameona nuru kuu, wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia. Umelikuza taifa, na kuzidisha furaha yao, wanafurahia mbele zako, kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani, umevunja nira iliyowalemea, ile gongo mabegani mwao na fimbo yake yeye aliyewaonea. Kila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani, na kila vazi lililovingirishwa katika damu vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa, vitakuwa kuni za kuwasha moto. Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanaume, nao utawala utakuwa mabegani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. Kuongezeka kwa utawala wake na amani hakutakuwa na mwisho. Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi na juu ya ufalme wake, akiuthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa adili, tangu wakati huo na hata milele. Wivu wa BWANA Mwenye Nguvu Zote utatimiza haya.