Isaya 8:16-20
Isaya 8:16-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Nitalihifadhi agizo hilo na kulifunga fundisho hilo miongoni mwa wafuasi wangu. Nitamngojea Mwenyezi-Mungu ambaye amejificha mbali na wazawa wa Yakobo; nitamtumainia. Mimi pamoja na watoto alionipa Mwenyezi-Mungu ni ishara na alama katika Israeli kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi akaaye mlimani Siyoni. Baadhi watawaambieni: “Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao, na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai.” Hakika anayesema hivyo hajapata kuona mwanga. Lakini nyinyi shikilieni lile agizo na fundisho la Mungu.
Isaya 8:16-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunge huo ushuhuda, ukaitie mhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia. Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni. Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi kulingana na neno hili, bila shaka kwa hao hakuna asubuhi.
Isaya 8:16-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia. Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni. Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong’ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.
Isaya 8:16-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria miongoni mwa wanafunzi wangu. Nitamngojea BWANA, ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake. Nitaliweka tumaini langu kwake. Niko hapa, pamoja na watoto ambao BWANA amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni. Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.