Isaya 8:11-15
Isaya 8:11-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema: “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina, usiogope kile wanachokiogopa, wala usikihofu. BWANA Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu, naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu, atakuwa mtego na tanzi. Wengi wao watajikwaa; wataanguka na kuvunjika, watategwa na kunaswa.”
Isaya 8:11-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alinionya kwa nguvu nisifuate njia za watu hawa, akaniambia, “Usijumuike nao katika njama zao, wala usiogope yale wanayoyaogopa wala kuwa na hofu. Nitambue mimi peke yangu, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kuwa mtakatifu; utaniogopa na kunicha mimi peke yangu. Mimi nitakuwa kimbilio, nitakuwa pia kama jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuziangusha falme za Israeli na Yuda; nitakuwa mtego wa kuwatega na kuwanasa wakazi wa Yerusalemu. Watu wengi watajikwaa, wataanguka na kupondeka; watanaswa katika mtego huo na kuchukuliwa mateka.”
Isaya 8:11-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana BWANA aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, Msiseme, Ni njama, kuhusu mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni njama; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.
Isaya 8:11-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana BWANA aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, Msiseme, Ni fitina, katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni fitina; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.