Isaya 65:17-25
Isaya 65:17-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha. Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao. Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia. Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema BWANA.
Isaya 65:17-25 Biblia Habari Njema (BHN)
“Sasa, naumba mbingu mpya na dunia mpya. mambo ya zamani hayatakumbukwa tena. Furahini, mkashangilie milele, kwa ajili ya vitu hivi ninavyoumba. Yerusalemu nitaufanya mji wa shangwe, na watu wake watu wenye furaha. Nami nitaufurahia mji wa Yerusalemu, nitawafurahia watu wangu. Sauti ya kilio haitasikika tena, kilio cha taabu hakitakuwako. Hakutakuwa tena na vifo vya watoto wachanga, wazee nao hawatakufa kabla ya wakati wao. Akifa mtu wa miaka 100 amekufa akiwa kijana; na akifa kabla ya miaka 100 ni balaa. Watu watajenga nyumba na kuishi humo; watalima mizabibu na kula matunda yake. Hawatajenga nyumba zikaliwe na watu wengine, wala kulima chakula kiliwe na watu wengine. Maana watu wangu niliowachagua wataishi maisha marefu kama miti; wateule wangu watafurahia matunda ya jasho lao. Kazi zao hazitakuwa bure, wala hawatazaa watoto wa kupata maafa; maana watakuwa waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu, wamebarikiwa wao pamoja na wazawa wao. Hata kabla hawajaniita, mimi nitawaitikia; kabla hawajamaliza kusema, nitakuwa nimewajibu. Mbwamwitu na kondoo watakula pamoja, simba watakula nyasi kama ng'ombe, nao nyoka chakula chao kitakuwa vumbi. Katika mlima wangu wote mtakatifu, hakuna atakayeumiza au kuharibu kitu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Isaya 65:17-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha. Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikika ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, kisha akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, kisha akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao. Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa bado wanena, nitasikia. Mbwamwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema BWANA.
Isaya 65:17-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Tazama, nitaumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa, wala hayatakuja akilini. Lakini furahini na kushangilia daima katika hivi nitakavyoumba, kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza, nao watu wake wawe furaha. Nami nitaifurahia Yerusalemu na kuwafurahia watu wangu; sauti ya maombolezo na ya kilio haitasikika humo tena. “Kamwe hatakuwepo tena ndani yake mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu, au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake. Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja atahesabiwa kwamba ni kijana tu, yeye ambaye hatafika miaka mia moja, atahesabiwa kuwa amelaaniwa. Watajenga nyumba na kuishi ndani yake; watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake. Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake, au kupanda mazao na wengine wale. Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti, ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi kazi za mikono yao. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga, kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na BWANA, wao na wazao wao pamoja nao. Kabla hawajaita, nitajibu, nao wakiwa katika kunena, nitasikia. Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, naye simba atakula nyasi kama maksai, lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote,” asema BWANA.