Isaya 58:7-11
Isaya 58:7-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usikose kumsaidia mtu aliye jamaa yako. Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na uponyaji wako utatokea punde; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimpa mtu mwenye njaa chakula chako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.
Isaya 58:7-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi, unapomwona aliye uchi, umvike, wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe? Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea upesi; ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako, na utukufu wa BWANA utakuwa mlinzi nyuma yako. Ndipo utaita, naye BWANA atajibu, utalia kuomba msaada, naye atasema: Mimi hapa. “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu, na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu, nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu na kutosheleza mahitaji ya walioonewa, ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani, nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri. BWANA atakuongoza siku zote, atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame, naye ataitia nguvu mifupa yako. Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri, kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
Isaya 58:7-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana. Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe.
Isaya 58:7-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.