Isaya 57:15-19
Isaya 57:15-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivi ndivyo asemavyo Mungu aliye juu kabisa, aishiye milele na ambaye jina lake ni “Mtakatifu”: “Mimi nakaa huko juu, mahali patakatifu, nakaa pia na wenye majuto na wanyenyekevu. Mimi nitawatia moyo walio wanyenyekevu na kuwapa nguvu wenye majuto. Maana sitaendelea kuwalaumu wala kuwakasirikia daima. La sivyo hao niliowaumba watadhoofika mbele yangu, nami ndiye niliyewapa pumzi yangu ya uhai. Niliwakasirikia kwa sababu ya uovu na tamaa zao; niliwaadhibu, nikauficha uso wangu na kukasirika. Lakini wao waliendelea kufuata njia zao wenyewe. Niliiona mienendo yao, lakini nitawaponya; nitawaongoza na kuwapa faraja, nitawatuliza hao wanaoomboleza. Mimi nitawapa amani, amani kwa walio mbali na walio karibu! Mimi nitawaponya.
Isaya 57:15-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu. Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya. Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake niliona hasira, nikampiga; nilificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe. Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia. Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema BWANA; nami nitamponya.
Isaya 57:15-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu. Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya. Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe. Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia. Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema BWANA; nami nitamponya.
Isaya 57:15-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu, lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu. Sitaendelea kulaumu milele, wala sitakasirika siku zote, kwa kuwa roho ya mwanadamu ingezimia mbele zangu: yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba. Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa. Nimeziona njia zake, lakini nitamponya, nitamwongoza na kumrudishia upya faraja, nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji katika Israeli. Amani, amani, kwa wale walio mbali na kwa wale walio karibu,” asema BWANA. “Nami nitawaponya.”