Isaya 55:1-9
Isaya 55:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
“Haya! Kila mwenye kiu na aje kwenye maji! Njoni, nyote hata msio na fedha; nunueni ngano mkale, nunueni divai na maziwa. Bila fedha, bila gharama! Mbona mnatumia fedha yenu kwa ajili ya kitu kisicho chakula? Ya nini kutoa jasho lenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni mimi kwa makini, nanyi mtakula vilivyo bora, na kufurahia vinono. “Tegeni sikio enyi watu wangu, mje kwangu; nisikilizeni, ili mpate kuishi. Nami nitafanya nanyi agano la milele; nitawapeni fadhili nilizomwahidi Daudi. Mimi nilimfanya kiongozi na kamanda wa mataifa ili yeye anishuhudie kwa watu wa mataifa. Sasa utayaita mataifa usiyoyajua, watu wa mataifa yasiyokutambua watakujia mbio, kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli niliyekufanya wewe utukuke.” Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu. Waovu na waache njia zao mbaya, watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya; wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia, wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mawazo yangu si kama mawazo yenu, wala njia zangu si kama njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo mbali na dunia, ndivyo njia zangu zilivyo mbali na zenu, na mawazo yangu mbali na mawazo yenu.
Isaya 55:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila gharama. Kwa nini mtoe fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono. Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara. Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa makabila ya watu; kuwa kiongozi na jemadari kwa makabila ya watu. Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya BWANA, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli; maana amekutukuza. Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yuko karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, ndivyo njia zangu zilivyo juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
Isaya 55:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani. Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono. Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara. Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu; kuwa kiongozi na jemadari kwa kabila za watu. Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya BWANA, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli; maana amekutukuza. Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
Isaya 55:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Njooni, ninyi nyote wenye kiu, njooni kwenye maji; nanyi ambao hamna fedha, njooni, nunueni na mle! Njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila gharama. Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, na kutaabikia kitu kisichoshibisha? Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono. Tegeni sikio mje kwangu, nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi. Nitafanya agano la milele nanyi, pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi. Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa, kiongozi na jemadari wa mataifa. Hakika utaita mataifa usiyoyajua, nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia, kwa sababu ya BWANA Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekutukuza.” Mtafuteni BWANA maadamu anapatikana; mwiteni maadamu yu karibu. Mtu mwovu na aiache njia yake, na mtu mbaya na ayaache mawazo yake. Yeye na amrudie BWANA, naye atamrehemu, arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa. “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu,” asema BWANA. “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia, ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.