Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 5:1-30

Isaya 5:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Nitaimba juu ya rafiki yangu, wimbo wa rafiki yangu na shamba lake la mizabibu: Rafiki yangu alikuwa na shamba la mizabibu juu ya kilima chenye rutuba nyingi. Alililima vizuri na kuondoa mawe yote, akaotesha humo mizabibu iliyochaguliwa; alijenga mnara wa ulinzi katikati yake, akachimba kisima cha kusindikia divai. Kisha akangojea lizae zabibu, lakini likazaa zabibu chungu. Kwa hiyo rafiki yangu anasema hivi: “Enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, amueni tafadhali kati yangu na shamba langu. Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu? Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri, mbona basi, likazaa zabibu chungu? “Na sasa nitawaambieni nitakavyolifanya hilo shamba langu. Nitauondoa ua wake, nalo litaharibiwa. Nitaubomoa ukuta wake, nalo litakanyagwakanyagwa. Nitaliacha liharibiwe kabisa, mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa. Litaota mbigili na miiba. Tena nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni jumuiya ya Waisraeli, na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda. Yeye alitazamia watende haki, badala yake wakafanya mauaji; alitazamia uadilifu, badala yake wakasababisha kilio! Ole wao wanaonunua nyumba baada ya nyumba, wanaoongeza mashamba juu ya mashamba yao, mpaka kila sehemu inakuwa mali yao, na hamna nafasi kwa wengine nchini. Nimemsikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi akitamka hivi: “Hakika nyumba nyingi zitabaki tupu, majumba makubwa mazuri bila wakazi. Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa lita nane tu za divai; anayepanda kilo 100 za mbegu atavuna kilo 10 tu za nafaka.” Ole wao wanaoamka asubuhi na mapema wapate kukimbilia kunywa kileo; wanaokesha hata usiku, mpaka divai iwaleweshe! Katika karamu zao, hapakosekani vinubi, zeze, matari, filimbi na divai. Lakini hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu, wala kuzitambua kazi za mikono yake. Kwa hiyo, watu wangu watapelekwa uhamishoni kwa sababu ya utovu wao wa akili. Watu wenu mashuhuri watakufa njaa, watu wengi watakufa kwa kiu. Kuzimu inawangoja kwa hamu kubwa, imepanua kinywa chake mpaka mwisho. Waheshimiwa pamoja na raia wa Yerusalemu wanaingia humo makundi kwa makundi, kadhalika na wote wanaousherehekea. Kila mtu atafedheheshwa, na wenye kiburi wote wataaibishwa. Lakini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatukuzwa. Yeye huonesha ukuu wake kwa matendo yake ya haki, kwa kuwahukumu watu wake. Wanakondoo, wanambuzi na ndama, watapata malisho yao kwenye magofu ya miji yao, kana kwamba hizo ni sehemu za malisho yao. Ole wao wanaoburuta uovu kama kwa kamba; wanaokokota dhambi kama kwa kamba za mkokoteni. Wanasema: “Mwache Mwenyezi-Mungu afanye haraka, tunataka kuyaona aliyosema atayafanya! Mtakatifu wa Israeli na atimize kusudi lake. Hebu na tuone ana mipango gani!” Ole wao wanaosema uovu ni wema na wema ni uovu. Giza wanasema ni mwanga na mwanga wanasema ni giza. Kichungu wanasema ni kitamu na kitamu wanakiona kuwa kichungu. Ole wao wanaojiona kuwa wenye hekima ambao wanajiona kuwa wenye akili. Ole wao mabingwa wa kunywa divai, hodari sana wa kuchanganya vileo. Kwa hongo kidogo wanawaachilia wenye hatia na kuwanyima wasio na hatia haki yao. Kwa hiyo, kama moto uteketezavyo nyasi, kama majani yateketeavyo katika mwali wa moto ndivyo na mizizi yao itakavyooza, na maua yao yatakavyopeperushwa juu kama vumbi. Maana wameiacha sheria ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi, wamedharau neno la yule Mtakatifu wa Israeli. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwawakia watu wake, akaunyosha mkono wake dhidi yao, akawachapa, hata milima ikatetemeka, maiti zao zikawa kama takataka katika barabara za mji. Hata hivyo, hasira yake haikutulia, mkono wake bado ameunyosha kuwaadhibu. Mwenyezi-Mungu analiashiria taifa la mbali; anawapigia mruzi watu kutoka miisho ya dunia; nao waja mbio na kuwasili haraka! Hawachoki wala hawajikwai; hawasinzii wala hawalali; hakuna mshipi wao uliolegea wala kamba ya kiatu iliyokatika. Mishale yao ni mikali sana, pinde zao zimevutwa tayari. Kwato za farasi wao ni ngumu kama mawe; mwendo wa magurudumu ya magari ni kimbunga. Askari wao wananguruma kama simba; wananguruma kama wanasimba ambao wamekamata mawindo yao na kuwapeleka mahali mbali ambapo hakuna awezaye kuwanyanganya. Siku hiyo, watanguruma juu ya Israeli kama mvumo wa bahari iliyochafuka. Atakayeiangalia nchi kavu ataona giza tupu na dhiki, mwanga utafunikwa na mawingu.

Shirikisha
Soma Isaya 5

Isaya 5:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio. Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi! BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu. Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu. Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao! Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya BWANA wala kuyafikiri matendo ya mikono yake. Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa, bali BWANA wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki. Ndipo wana-kondoo watakapolisha kama katika malisho yao wenyewe, na mahali pao waliowanda, palipoachwa ukiwa, wageni watakula. Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari! Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona. Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu! Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe! Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo; wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake! Kwa hiyo kama vile mwali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika mwali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli. Kwa sababu hiyo hasira ya BWANA imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Naye atawatwekea bendera mataifa toka mbali, Naye atawapigia miunzi tokea mwisho wa nchi; Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana. Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pindi zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli; Ngurumo yao itakuwa kama ya simba; Watanguruma kama wana-simba; Naam, watanguruma na kukamata mateka, Na kuyachukua na kwenda zao salama, Wala hakuna mtu atakayeokoa. Nao watanguruma juu yao siku hiyo Kama ngurumo ya bahari; Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake.

Shirikisha
Soma Isaya 5

Isaya 5:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu kuhusu shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akachimba handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibumwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyohitajika kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibumwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa ua wake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio. Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hadi ikawa hapana nafasi tena, nanyi ikawa hamna budi kukaa peke yenu katikati ya nchi! BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu. Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu. Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hadi usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao! Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya BWANA wala kuyafikiri matendo ya mikono yake. Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa, bali BWANA wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki. Ndipo wana-kondoo watakapojilisha kama walio katika malisho yao wenyewe, na mahali pao walionenepa, palipoachwa ukiwa, wageni watakula. Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari! Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona. Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu! Ole wao walio na hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe! Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, na walio hodari wa kuchanganya vileo; wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake! Kwa hiyo kama vile muali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika muali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli. Kwa sababu hiyo hasira ya BWANA imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. Naye atawatolea ishara mataifa toka mbali, Naye atawapigia miruzi tokea mwisho wa nchi; Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana. Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pinde zao zote zimepindika; Kwato za farasi wao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli; Ngurumo yao itakuwa kama ya simba; Watanguruma kama wanasimba; Naam, watanguruma na kukamata mateka, Na kuyachukua na kwenda zao salama, Wala hakuna mtu atakayeokoa. Nao watanguruma juu yao siku hiyo Kama ngurumo ya bahari; Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake.

Shirikisha
Soma Isaya 5

Isaya 5:1-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye, kuhusu shamba lake la mizabibu: Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu kwenye kilima chenye rutuba. Alililima na kuondoa mawe na akaliotesha mizabibu bora sana. Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake, na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia. Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri, lakini lilizaa matunda mabaya tu. “Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu. Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika kwa shamba langu la mizabibu kuliko yale niliyofanya? Nilipotazamia kupata zabibu nzuri, kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu? Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea shamba langu la mizabibu: Nitaondoa uzio wake, nalo litaharibiwa, nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa. Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu, halitakatiwa matawi wala kulimwa, nayo michongoma na miiba itamea huko, nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” Shamba la mzabibu la BWANA Mwenye Nguvu Zote ni nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni bustani yake ya kumpendeza. Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu, alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu. Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi. BWANA Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa. Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja ya divai, na homeri ya mbegu zilizopandwa itatoa efa moja tu ya nafaka.” Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana mpaka usiku, mpaka wamewaka kwa mvinyo. Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya BWANA, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake. Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa ufahamu, watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa na watu wao wengi watakauka kwa kiu. Kwa hiyo kaburi limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote. Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa. Lakini BWANA Mwenye Nguvu Zote atatukuzwa kwa ajili ya haki yake, naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa haki yake. Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe, wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri. Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu na uovu kama kwa kamba za mkokoteni, kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka, aharakishe kazi yake ili tupate kuiona. Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike, tena udhihirike ili tupate kuujua.” Ole wao wanaoita ubaya ni wema, na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu. Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe, na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe. Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo, nao walio hodari katika kuchanganya vileo, wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia. Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi, na kama vile majani makavu yazamavyo katika miali ya moto, ndivyo mizizi yao itakavyooza na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi; kwa kuwa wameikataa sheria ya BWANA Mwenye Nguvu Zote na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli. Kwa hiyo hasira ya BWANA inawaka dhidi ya watu wake, mkono wake umeinuliwa na anawapiga. Milima inatetemeka, maiti ni kama takataka kwenye barabara. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali, anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia. Tazama wamekuja, kwa kasi na kwa haraka! Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa, hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala, hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni, hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika. Mishale yao ni mikali, pinde zao zote zimevutwa, kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume, magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli. Ngurumo yao ni kama ile ya simba, wananguruma kama wana simba, wanakoroma wanapokamata mawindo yao, na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa. Katika siku ile watanguruma juu yake kama ngurumo za bahari. Kama mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki; hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.

Shirikisha
Soma Isaya 5