Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 43:1-28

Isaya 43:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo, yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema: “Msiogope, maana mimi nimewakomboa; nimewaita kwa jina nanyi ni wangu. Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza. Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu. Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu, nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru. Kwa vile mna thamani mbele yangu, kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda, mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi, nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu. Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi. “Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki, nitawakusanyeni kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’, na kusini, ‘Usiwazuie’! Warudisheni watu kutoka mbali, kutoka kila mahali duniani. Kila mmoja hujulikana kwa jina langu, niliwaumba wote na kuwafanya kwa ajili ya utukufu wangu.” Waleteni mbele watu hao, ambao wana macho lakini hawaoni wana masikio lakini hawasikii! Mataifa yote na yakusanyike, watu wote na wakutane pamoja. Nani kati ya miungu yao awezaye kutangaza yatakayotukia? Nani awezaye kutuonesha yanayotukia sasa? Wawalete mashahidi wao kuthibitisha kwamba walifanya hivyo. Waache wasikilize na kusema, “Ilikuwa kweli.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi Waisraeli ni mashahidi wangu; niliwachagua muwe watumishi wangu, mpate kunijua na kuniamini, kwamba ndimi peke yangu Mungu. Kabla yangu hajapata kuwapo mungu mwingine, wala hatakuwapo mungu mwingine. “Mimi peke yangu ndimi Mwenyezi-Mungu, hakuna mkombozi mwingine ila mimi. Nilitangaza yale ambayo yangetukia, kisha nikaja na kuwakomboa. Hakuna mungu mwingine aliyewahi kufanya hivyo, nanyi ni mashahidi wangu. Mimi ni Mungu na nitakuwa Mungu daima. Hakuna awezaye kuiepa nguvu yangu; hakuna awezaye kupinga ninayofanya.” Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi: “Kwa ajili yenu nitatuma jeshi Babuloni. Nitayavunjilia mbali malango ya mji wake, na kelele za hao Wakaldayo zitageuka maombolezo. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wenu; Mimi ndimi Muumba wa Israeli, Mfalme wenu.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wakati mmoja nilifanya barabara baharini nikaweka njia kati ya mawimbi makubwa. Nililipiga jeshi lenye nguvu, jeshi la magari na farasi wa vita, askari na mashujaa wa vita. Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena, niliwakomesha na kuwazima kama utambi wa taa. Sasa nasema: ‘Msiyanganganie mambo yaliyopita, wala msifikirie vitu vya zamani. Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya. Kinafanyika sasa hivi, nanyi mtaweza kukiona. Nitafanya njia nyikani, na kububujisha mito jangwani. Wanyama wa porini wataniheshimu, kina mbweha na kina mbuni, maana nitaweka maji nyikani, na kububujisha mito jangwani, ili kuwanywesha watu wangu wateule, watu niliowaumba kwa ajili yangu mwenyewe, ili wazitangaze sifa zangu!’ “Lakini ewe taifa la Yakobo, hukuniabudu mimi; enyi watu wa Israeli, mlinichoka mimi! Hamjaniletea kondoo wenu wa sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa tambiko zenu. Nami sikuwalemeza kwa kutaka sadaka, wala sikuwachosha kwa kuwadai ubani. Hamkuninunulia manukato kwa faida yenu, wala kuniridhisha kwa nyama nono za tambiko. Badala yake dhambi zenu zimekuwa mzigo kwangu, mmenichosha kabisa kwa makosa yenu. Walakini mimi ndimi niliyefuta makosa yenu kwa heshima yangu, ndimi niyafutaye makosa kwa ajili yangu mwenyewe, na wala sitazikumbuka dhambi zenu. “Niambie kama mna kisa nami, njoo tukahojiane; toeni mashtaka yenu ili tuuone ukweli wenu! Babu yenu wa kwanza alitenda dhambi, wapatanishi wenu waliniasi. Kwa hiyo niliwafanya haramu wakuu wa mahali patakatifu nikawaacha watu wa Yakobo waangamizwe, naam, nikawaacha Waisraeli watukanwe.”

Shirikisha
Soma Isaya 43

Isaya 43:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio. Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli. Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia? BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu. BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu. Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli. Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani. Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi. Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.

Shirikisha
Soma Isaya 43

Isaya 43:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Lakini sasa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyekuumba, ee Yakobo, yeye aliyekuhuluku, ee Israeli: “Usiogope kwa maana nimekukomboa, nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu. Unapopita kwenye maji makuu, nitakuwa pamoja nawe, unapopita katika mito ya maji, hayatakugharikisha. Utakapopita katika moto, hutaungua, miali ya moto haitakuunguza. Kwa kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako. Ninaitoa Misri kuwa fidia yako, Kushi na Seba badala yako. Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu, nami kwa kuwa ninakupenda, nitatoa watu badala yako na mataifa badala ya maisha yako. Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe, nitawaleta watoto wako kutoka mashariki, na kukukusanya kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’ nayo kusini, ‘Usiwazuie.’ Walete wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia: kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemuumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.” Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni, wenye masikio lakini hawasikii. Mataifa yote yanakutanika pamoja, na makabila yanakusanyika. Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya, na kututangazia mambo yaliyopita? Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi, ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.” “Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA, “na mtumishi wangu niliyemchagua, ili mpate kunijua na kuniamini, na kutambua kwamba Mimi ndiye. Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa, wala hatakuwepo mwingine baada yangu. Mimi, naam mimi, ndimi BWANA, zaidi yangu hakuna mwokozi. Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza: Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu. Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA, “kwamba Mimi ndimi Mungu. Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye. Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa kutoka mkononi wangu. Mimi ninapotenda, ni nani awezaye kutangua?” Hili ndilo BWANA asemalo, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa ajili yenu nitatumana Babeli na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi, katika meli walizozionea fahari. Mimi ndimi BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wako, Muumba wa Israeli, Mfalme wako.” Hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyefanya njia baharini, mahali pa kupita kwenye maji mengi, aliyeyakokota magari ya vita na farasi, jeshi pamoja na askari wa msaada, nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe, wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi: “Msiyakumbuke mambo yaliyopita, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitafanya jambo jipya! Sasa litachipuka, je, hamtalitambua? Nitafanya njia jangwani na vijito vya maji katika nchi kame. Wanyama wa mwituni wataniheshimu, mbweha na bundi, kwa sababu ninawapatia maji jangwani, na vijito katika nchi kame, ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua, watu wale niliowaumba kwa ajili yangu, ili wapate kutangaza sifa zangu. “Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo, hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli. Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukulemea kwa sadaka za nafaka wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba. Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato, wala hukunipa kwa ukarimu mafuta ya wanyama wa dhabihu zako. Lakini umenilemea kwa dhambi zako, na kunitaabisha kwa makosa yako. “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako, kwa ajili yangu mwenyewe, wala sizikumbuki dhambi zako tena. Tafakari mambo yaliyopita, njoo na tuhojiane, leta shauri lako uweze kupewa haki yako. Baba yako wa kwanza alitenda dhambi, wasemaji wako wameasi dhidi yangu. Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako, nami nitamtoa Yakobo aangamizwe, na Israeli adhihakiwe.

Shirikisha
Soma Isaya 43

Isaya 43:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na makabila ya watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. Walete watu wasioona, japo wana macho, wasiosikia japo wana masikio. Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli. Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hakuna awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia? BWANA, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni BWANA, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu. BWANA asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa kama utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama pori wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu. Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli. Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani. Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako. Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi. Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.

Shirikisha
Soma Isaya 43

Isaya 43:1-28

Isaya 43:1-28 BHNIsaya 43:1-28 BHNIsaya 43:1-28 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima