Isaya 43:1-13
Isaya 43:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na makabila ya watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. Walete watu wasioona, japo wana macho, wasiosikia japo wana masikio. Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli. Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hakuna awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?
Isaya 43:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio. Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli. Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?
Isaya 43:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo, yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema: “Msiogope, maana mimi nimewakomboa; nimewaita kwa jina nanyi ni wangu. Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza. Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu. Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu, nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru. Kwa vile mna thamani mbele yangu, kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda, mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi, nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu. Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi. “Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki, nitawakusanyeni kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’, na kusini, ‘Usiwazuie’! Warudisheni watu kutoka mbali, kutoka kila mahali duniani. Kila mmoja hujulikana kwa jina langu, niliwaumba wote na kuwafanya kwa ajili ya utukufu wangu.” Waleteni mbele watu hao, ambao wana macho lakini hawaoni wana masikio lakini hawasikii! Mataifa yote na yakusanyike, watu wote na wakutane pamoja. Nani kati ya miungu yao awezaye kutangaza yatakayotukia? Nani awezaye kutuonesha yanayotukia sasa? Wawalete mashahidi wao kuthibitisha kwamba walifanya hivyo. Waache wasikilize na kusema, “Ilikuwa kweli.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi Waisraeli ni mashahidi wangu; niliwachagua muwe watumishi wangu, mpate kunijua na kuniamini, kwamba ndimi peke yangu Mungu. Kabla yangu hajapata kuwapo mungu mwingine, wala hatakuwapo mungu mwingine. “Mimi peke yangu ndimi Mwenyezi-Mungu, hakuna mkombozi mwingine ila mimi. Nilitangaza yale ambayo yangetukia, kisha nikaja na kuwakomboa. Hakuna mungu mwingine aliyewahi kufanya hivyo, nanyi ni mashahidi wangu. Mimi ni Mungu na nitakuwa Mungu daima. Hakuna awezaye kuiepa nguvu yangu; hakuna awezaye kupinga ninayofanya.”
Isaya 43:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini sasa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyekuumba, ee Yakobo, yeye aliyekuhuluku, ee Israeli: “Usiogope kwa maana nimekukomboa, nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu. Unapopita kwenye maji makuu, nitakuwa pamoja nawe, unapopita katika mito ya maji, hayatakugharikisha. Utakapopita katika moto, hutaungua, miali ya moto haitakuunguza. Kwa kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako. Ninaitoa Misri kuwa fidia yako, Kushi na Seba badala yako. Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu, nami kwa kuwa ninakupenda, nitatoa watu badala yako na mataifa badala ya maisha yako. Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe, nitawaleta watoto wako kutoka mashariki, na kukukusanya kutoka magharibi. Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’ nayo kusini, ‘Usiwazuie.’ Walete wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia: kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemuumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.” Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni, wenye masikio lakini hawasikii. Mataifa yote yanakutanika pamoja, na makabila yanakusanyika. Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya, na kututangazia mambo yaliyopita? Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi, ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.” “Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA, “na mtumishi wangu niliyemchagua, ili mpate kunijua na kuniamini, na kutambua kwamba Mimi ndiye. Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa, wala hatakuwepo mwingine baada yangu. Mimi, naam mimi, ndimi BWANA, zaidi yangu hakuna mwokozi. Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza: Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu. Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA, “kwamba Mimi ndimi Mungu. Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye. Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa kutoka mkononi wangu. Mimi ninapotenda, ni nani awezaye kutangua?”