Isaya 38:1-6
Isaya 38:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA, akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.
Isaya 38:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.” Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana. Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya: “Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.”
Isaya 38:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa karibu kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA, akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia kwa uchungu. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Nenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, kutoka kwa mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.
Isaya 38:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo BWANA: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.” Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA: “Ee BWANA, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu. Ndipo neno la BWANA likamjia Isaya, kusema: “Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.