Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 34:1-17

Isaya 34:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Karibieni mkasikilize enyi mataifa, tegeni sikio enyi watu. Sikiliza ee dunia na vyote vilivyomo, ulimwengu na vyote vitokavyo humo! Mwenyezi-Mungu ameyakasirikia mataifa yote, ameghadhabika dhidi ya majeshi yao yote. Ameyapangia mwisho wao, ameyatoa yaangamizwe. Maiti zao zitatupwa nje; harufu ya maiti zao itasambaa; milima itatiririka damu yao. Jeshi lote la angani litaharibika, anga zitakunjamana kama karatasi. Jeshi lake lote litanyauka, kama majani ya mzabibu yanyaukavyo, naam, kama tunda la mtini linyaukavyo. Upanga wa Mungu uko tayari juu mbinguni. Tazama, washuka kuwaadhibu Waedomu, watu ambao ameamua kuwaangamiza. Upanga utalowa damu na kutapakaa mafuta, kama kwa damu ya kondoo na mbuzi, na mafuta ya figo za kondoo dume. Maana Mwenyezi-Mungu atatoa kafara huko Bosra, kutakuwa na mauaji makubwa nchini Edomu. Nyati wataangamia pamoja nao, ndama kadhalika na mafahali. Nchi italoweshwa damu, udongo utarutubika kwa mafuta yao. Maana Mwenyezi-Mungu anayo siku ya kisasi; mwaka wa kulipiza maadui wa Siyoni. Vijito vya Edomu vitatiririka lami, udongo wake utakuwa madini ya kiberiti; ardhi yake itakuwa lami iwakayo. Itawaka usiku na mchana bila kuzimika, moshi wake utafuka juu milele. Nchi itakuwa jangwa siku zote, hakuna atakayepitia huko milele. Itakuwa makao ya kozi na nungunungu, bundi na kunguru wataishi humo. Mwenyezi-Mungu atawaletea ghasia, na timazi la fujo kwa wakuu wake. Nchi itaitwa “Nchi bila Mfalme;” wakuu wake wote wametoweka. Miiba itaota katika ngome zake, viwavi na michongoma mabomani mwao. Itakuwa makao ya mbwamwitu, maskani yao mbuni. Pakamwitu na fisi watakuwa humo, majini yataitana humo; kwao usiku utakuwa mwanga, na humo watapata mahali pa kupumzikia. Humo bundi watataga mayai na kuyaatamia, wataangua vifaranga na kuviweka kivulini mwao. Humo vipanga watakutania, kila mmoja na mwenzake. Someni katika kitabu cha Mwenyezi-Mungu: “Hakuna hata kiumbe kimoja kitakachokosekana, kila kimoja kitakuwako na mwenzake.” Maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hivyo, roho yake itawakusanya hao wote. Mwenyezi-Mungu amepanga sehemu ya kila mmoja wao, ametumia kamba kuwapimia nchi hiyo; wataimiliki milele na milele, wataishi humo kizazi hata kizazi.

Shirikisha
Soma Isaya 34

Isaya 34:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Njooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize; sikilizeni kwa makini, enyi kabila za watu! Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake, ulimwengu na vyote vitokavyo ndani yake! BWANA ameyakasirikia mataifa yote; ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote. Atawaangamiza kabisa, atawatia mikononi mwa wachinjaji. Waliouawa watatupwa nje, maiti zao zitatoa uvundo, milima itatota kwa damu zao. Nyota zote za mbinguni zitayeyuka na anga litasokotwa kama kitabu, jeshi lote la angani litaanguka kama majani yaliyonyauka kutoka kwenye mzabibu, kama tini iliyonyauka kutoka kwenye mtini. Upanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni, tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu, wale watu ambao nimeshawahukumu, kuwaangamiza kabisa. Upanga wa BWANA umeoga katika damu, umefunikwa na mafuta ya nyama: damu ya kondoo na mbuzi, mafuta kutoka figo za kondoo dume. Kwa maana BWANA ana dhabihu huko Bosra, na machinjo makuu huko Edomu. Nyati wataanguka pamoja nao, ndama waume na mafahali wakubwa. Nchi yao italowana kwa damu, nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama. Kwa sababu BWANA anayo siku ya kulipiza kisasi, mwaka wa malipo, siku ya kushindania shauri la Sayuni. Vijito vya Edomu vitageuka kuwa lami, mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho, nchi yake itakuwa lami iwakayo! Haitazimishwa usiku wala mchana, moshi wake utapaa juu milele. Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa, hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena. Bundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki, bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo. Mungu atanyoosha juu ya Edomu kamba ya kupimia ya machafuko matupu, na timazi ya ukiwa. Watu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote kitakachoitwa ufalme huko, nao wakuu wao wote watatoweka. Miiba itaenea katika ngome za ndani, viwawi na michongoma itaota kwenye ngome zake. Itakuwa maskani ya mbweha, makao ya bundi. Viumbe vya jangwani vitakutana na fisi, nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana; huko viumbe vya usiku vitastarehe pia na kujitafutia mahali pa kupumzika. Bundi wataweka viota huko na kutaga mayai, atayaangua na kutunza makinda yake chini ya uvuli wa mabawa yake; pia huko vipanga watakusanyika, kila mmoja na mwenzi wake. Angalieni katika gombo la BWANA na msome: Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana, hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake. Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza, na Roho wake atawakusanya pamoja. Huwagawia sehemu zao, mkono wake huwagawanyia kwa kipimo. Wataimiliki hata milele na kuishi humo kutoka kizazi hadi kizazi.

Shirikisha
Soma Isaya 34

Isaya 34:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi makabila ya watu; dunia na isikie, na chote kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo. Maana BWANA ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa. Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao. Na jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi, na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika. Maana upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu. Oba 1-14; Mal 1:2-5 Upanga wa BWANA umeshiba damu, umejazwa mafuta, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo dume; maana BWANA ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu. Na nyati watateremka pamoja nao, na ndama pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu. Maana ni siku ya kisasi cha BWANA, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni. Na vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo. Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele; tangu kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele. Kozi na nungunungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu. Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu. Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni. Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwamwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kupata pahali pa kustarehe. Huko bundi atajenga kiota chake na kutaga mayai na kuyaatamia, na kuangua, na kukusanya vifaranga wake katika kivuli chake; naam, huko watakusanyika tai, kila mmoja na mwenzake. Tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya. Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.

Shirikisha
Soma Isaya 34

Isaya 34:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi kabila za watu; dunia na isikie, nacho kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo. Maana BWANA ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa. Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao. Na jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi, na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika. Maana upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu. Oba 1-14; Mal 1:2-5 Upanga wa BWANA umeshiba damu, umenona kwa unono, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo waume; maana BWANA ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu. Na nyati watatelemka pamoja nao, na mahasai pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu. Maana ni siku ya kisasi cha BWANA, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni. Na vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo. Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele; tangu kizazi hata kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele. Kaati na nungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu. Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu. Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni. Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwa-mwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kujipatia raha. Huko pili atafanya kioto chake na kuzaa na kuotamia, na kukusanya watoto wake katika kivuli chake; naam, huko watakusanyika tai, kila mmoja na mwenzake. Tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya. Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.

Shirikisha
Soma Isaya 34