Isaya 28:1-6
Isaya 28:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka! Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba; na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia! Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu, ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali, kama tufani ya mafuriko makubwa; kwa mkono wake atawatupa chini ardhini. Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu yatakanyagwakanyagwa ardhini, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka; fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi; mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja. Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu, kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai. Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki, nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
Isaya 28:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wa taji la kiburi la walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai! Tazama, Bwana ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, tufani iharibuyo, kama dhoruba ya maji mengi yafurikayo, ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono. Taji la kiburi la walevi wa Efraimu litakanyagwa kwa miguu; na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa joto, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake. Katika siku ile BWANA wa majeshi atakuwa ni taji la fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake. Naye atakuwa roho ya hukumu ya haki kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao walindao langoni.
Isaya 28:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wa taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai! Tazama, Bwana ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, tufani iharibuyo, kama dhoruba ya maji mengi yafurikayo, ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono. Taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu itakanyagwa kwa miguu; na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa hari, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake. Katika siku ile BWANA wa majeshi atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake. Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni.
Isaya 28:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu, kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba: kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo! Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu. Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo, kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo, atakiangusha chini kwa nguvu. Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu, kitakanyagwa chini ya nyayo. Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba, litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno: mara mtu aionapo, huichuma na kuila. Katika siku ile, BWANA Mwenye Nguvu Zote atakuwa taji la utukufu, taji zuri la maua kwa mabaki ya watu wake. Atakuwa roho ya haki kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu, chanzo cha nguvu kwa wale wazuiao vita langoni.