Isaya 2:12-22
Isaya 2:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Naam, yaja siku ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi dhidi ya wenye kiburi na majivuno, dhidi ya wote wanaojikweza; dhidi ya mierezi yote ya Lebanoni, ambayo ni mirefu na mizuri, dhidi ya mialoni yote nchini Bashani; dhidi ya milima yote mirefu, dhidi ya vilima vyote vya juu; dhidi ya minara yote mirefu, dhidi ya kuta zote za ngome; dhidi ya meli zote za Tarshishi, na dhidi ya meli zote nzuri. Kiburi chote cha watu kitakomeshwa, majivuno ya kila mtu yatavunjwa. Na Mwenyezi-Mungu peke yake atatukuzwa siku hiyo. Vinyago vyote vya miungu vitatoweka kabisa. Ingieni katika mapango miambani, katika mashimo ardhini, kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu, mbali na utukufu wa enzi yake, atakapokuja kuitia hofu dunia. Siku hiyo, watu watawatupia panya na popo vinyago vyao vya fedha na dhahabu walivyojitengenezea ili kuviabudu. Nao wataingia katika mapango miambani na kwenye nyufa za miamba, kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu, mbali na utukufu wa enzi yake, atakapokuja kuitia hofu dunia. Usimwamini binadamu, uhai wake haudumu kama pumzi. Yeye anafaa kitu gani?
Isaya 2:12-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini. Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani; na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka; na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma; na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo. Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Nazo sanamu zitatoweka kabisa. Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo; ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. Mwacheni mwanadamu ambaye pumzi yake i katika mianzi ya pua yake; kwa maana hudhaniwaje kuwa ni kitu?
Isaya 2:12-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa), kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana, na mialoni yote ya Bashani, kwa milima yote mirefu na vilima vyote vilivyoinuka, kwa kila mnara ulio mrefu sana na kila ukuta wenye ngome, kwa kila meli ya biashara, na kila chombo cha baharini cha fahari. Majivuno ya mwanadamu yatashushwa, na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa, BWANA peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo, nazo sanamu zitatoweka kabisa. Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba, na kwenye mahandaki ardhini kutokana na utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia. Siku ile, watu watawatupia panya na popo sanamu zao za fedha na za dhahabu, walizozitengeneza ili waziabudu. Watakimbilia kwenye mapango miambani na kwenye nyufa za miamba kutokana na utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia. Acheni kumtumainia mwanadamu, ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake. Yeye ana thamani gani?
Isaya 2:12-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini. Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani; na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka; na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma; na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo. Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Nazo sanamu zitatoweka kabisa. Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojitengenezea ili kuziabudu, kwa fuko na popo; ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa BWANA na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. Mwacheni mwanadamu ambaye pumzi yake iko katika mianzi ya pua yake; kwa maana wanafaa kitu gani?