Isaya 2:1-5
Isaya 2:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno alilopewa Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na Yerusalemu. Siku zijazo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu utaimarishwa kupita milima yote, utainuliwa juu ya vilima vyote. Mataifa yote yatamiminika huko, watu wengi wataujia na kusema, “Njoni tupande mlima wa Mwenyezi-Mungu, twende nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, apate kutufundisha njia zake, nasi tuishi kadiri ya mwongozo wake. Maana sheria itakuja kutoka Siyoni; neno la Mwenyezi-Mungu kutoka Yerusalemu.” Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa atakata mashauri ya watu wengi. Watu watafua panga za vita kuwa majembe na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea. Taifa halitapigana na taifa lingine wala hayatafanya tena mazoezi ya vita. Sasa, enyi wazawa wa Yakobo, njoni, tutembee katika mwanga wa Mwenyezi-Mungu.
Isaya 2:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya BWANA.
Isaya 2:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya BWANA.
Isaya 2:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu: Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la BWANA utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko. Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni mlimani mwa BWANA, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Sheria itatoka Sayuni, neno la BWANA litatoka Yerusalemu. Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena. Njooni, enyi nyumba ya Yakobo, tutembeeni katika nuru ya BWANA.