Isaya 11:10-16
Isaya 11:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka. Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani. Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa, kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa, kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa, na kuwarudisha toka pembe nne za dunia. Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma, hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu. Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi, pamoja watawapora watu wakaao mashariki. Watawashinda Waedomu na Wamoabu, nao Waamoni watawatii. Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu, kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate, nao utagawanyika katika vijito saba, watu wavuke humo miguu mikavu. Tena, kutakuwa na barabara kuu toka Ashuru kwa ajili ya watu wake waliobaki humo kama ilivyokuwa kwa Waisraeli wakati walipotoka nchini Misri.
Isaya 11:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa makabila ya watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu. Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari. Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia. Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu. Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii. Na BWANA atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu waliovaa viatu bila kulowa. Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.
Isaya 11:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu. Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari. Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia. Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu. Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii. Na BWANA atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu. Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.
Isaya 11:10-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu. Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi, na kutoka visiwa vya baharini. Atainua bendera kwa mataifa na kuwakusanya Waisraeli walio uhamishoni; atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika kutoka pembe nne za dunia. Wivu wa Efraimu utatoweka, na adui wa Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamwonea Yuda wivu, wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu. Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti hadi upande wa magharibi, kwa pamoja watawateka watu nyara hadi upande wa mashariki. Watawapiga Edomu na Moabu, na Waamoni watatawaliwa nao. Mwenyezi Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Misri; kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake juu ya Mto Frati. Ataugawanya katika vijito saba ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu. Kutakuwa na njia kuu kwa mabaki ya watu wake wale waliosalia kutoka Ashuru, kama ilivyokuwa kwa Israeli walipopanda kutoka Misri.