Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 10:5-34

Isaya 10:5-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme? Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake? Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake. Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu. Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea BWANA, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli. Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu. Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki. Kwa maana Bwana, BWANA wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri. Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza. Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri. Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta. Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi; wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia. Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi! Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie; siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu. Angalia, Bwana, BWANA wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini; naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza.

Shirikisha
Soma Isaya 10

Isaya 10:5-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wake Ashuru, fimbo ya hasira yangu, yeye ashikaye kiboko cha hasira yangu! Nilimtuma kuliadhibu taifa ovu, nilimwamuru kuwaadhibu watu niliowakasirikia, kuwapora na kuteka nyara, na kuwakanyaga chini kama tope njiani. Lakini Ashuru hakudhamiria hivyo, yeye alikuwa na nia nyingine; alikusudia kuharibu kabisa, kuangamiza mataifa mengi iwezekanavyo. Maana alisema: “Je, si kweli majemadari wangu ni wafalme? Je, si kweli kwamba Kalno nitautenda kama Karkemishi, mji wa Hamathi kama mji wa Arpadi, Samaria kama Damasko? Kama nimefaulu kuunyosha mkono wangu dhidi ya falme zenye sanamu za miungu kubwa kuliko sanamu za Yerusalemu na Samaria; je, nitashindwa kuutenda Yerusalemu na sanamu zake, kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?” Wakati Mwenyezi-Mungu atakapomaliza kazi zake zote mlimani Siyoni na mjini Yerusalemu, atamwadhibu mfalme wa Ashuru, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake. Maana mfalme wa Ashuru alisema: “Kwa nguvu zangu mwenyewe nimetenda hayo, na kwa hekima yangu, maana mimi ni mwerevu! Nimeondoa mipaka kati ya mataifa, nikazipora hazina zao; kama fahali nimewaporomosha walioketia viti vya enzi. Kama mtu anyoshaye mkono kwenye kiota, ndivyo nilivyochukua mali yao; kama mtu aokotavyo mayai yaliyoachwa kiotani, ndivyo nilivyowaokota duniani kote, wala hakuna mtu aliyeweza kupiga bawa, au aliyefungua kinywa kunipigia kelele.” Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, shoka litajigamba dhidi ya anayelitumia? Msumeno waweza kujivuna dhidi ya mwenye kukata nao? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua anayeishika, au mkongojo kumwinua mwenye kuutumia!” Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atawaletea askari wao ugonjwa wa kuwakondesha, na fahari yao itateketezwa kama kwa moto. Mungu aliye mwanga wa Israeli atakuwa kama moto, Mtakatifu wa Israeli atakuwa mwali wa moto ambao kwa siku moja utateketeza kila kitu: Miiba yake na mbigili zake pamoja. Misitu yake ya fahari na mashamba yake mazuri, Mwenyezi-Mungu atayaangamiza yote; itakuwa kama mtu aliyemalizwa na ugonjwa. Miti itakayobaki msituni mwake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo ataweza kuihesabu. Siku ile wazawa wa Yakobo watakaobaki, naam, Waisraeli watakaosalia hawatalitegemea tena taifa lililowaadhibu, bali watamtegemea kabisa Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. Wazawa wa Yakobo wachache watakaobaki watamrudia Mungu Mkuu. Maana, hata kama sasa Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaorudi. Maangamizi yamepangwa yafanyike, nayo yatafanyika kwa haki tupu. Naam! Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atakamilisha kabisa katika nchi yote jambo aliloamua kutenda. Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi watu wangu mnaokaa Siyoni msiwaogope Waashuru ambao wanawapiga kwa fimbo, wakiinua mikongojo yao dhidi yenu kama walivyofanya Wamisri. Maana bado kitambo, nayo hasira yangu itapita na ghadhabu yangu itawageukia Waashuru. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi na nitawachapa kama nilivyowachapa Wamidiani kwenye jabali la Orebu. Nitanyosha fimbo yangu juu ya bahari kuwachapa kama nilivyowafanya Wamisri. Wakati huo, mzigo waliowabebesha nitauondoa na nira waliyowatia shingoni mwenu itavunjwa.” Adui amepanda kutoka Rimoni, amefika mjini Ayathi. Amepitia huko Migroni, mizigo yake ameiacha Mikmashi. Amekwisha pita kivukoni, usiku huu analala Geba. Watu wa Rama wanatetemeka kwa hofu, wakazi wa Gibea, mji wa Shauli, wamekimbia. Pazeni sauti enyi watu wa Galimu! Tegeni sikio enyi watu wa Laisha! Jibuni enyi wenyeji wa Anathothi! Watu wa Madmena wako mbioni, wakazi wa Gebimu wanakimbilia usalama. Leo hii, adui atatua Nobu, atatikisa ngumi yake dhidi ya mlima Siyoni; naam, atautikisia ngumi mji wa Yerusalemu. Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakata matawi yake kwa ukatili; miti mirefu itaangushwa chini, walio juu wataaibishwa. Atakata vichaka vya msituni kwa shoka, Lebanoni na mierezi yake maarufu itaanguka.

Shirikisha
Soma Isaya 10

Isaya 10:5-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme? Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyofikia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake? Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitamwadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake. Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kiota cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atatuma maradhi ya kukondesha kwa wapiganaji walionenepa; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa muali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake kwa siku moja. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu. Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea BWANA, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli. Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu. Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki. Kwa maana Bwana, BWANA wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote. Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kama walivyofanya Wamisri. Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza. Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kama walivyofanya Wamisri. Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta. Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi; wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia. Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi! Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie; siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu. Angalia, Bwana, BWANA wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini; naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza.

Shirikisha
Soma Isaya 10

Isaya 10:5-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu! Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani. Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi. Maana asema, ‘Je, wafalme wote si majemadari wangu? Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi, nayo Samaria si kama Dameski? Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria: je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake kama nilivyoshughulikia Samaria na vinyago vyake?’ ” Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao. Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ” Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia! Kwa hiyo Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto. Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake. Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo. Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu. Katika siku ile, mabaki ya Israeli, walionusurika wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, lakini watamtegemea kwa kweli BWANA Aliye Mtakatifu wa Israeli. Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo watamrudia Mungu Mwenye Nguvu. Ingawa watu wako, ee Israeli, ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaorudi. Maangamizi yamekwisha amriwa, ni mengi tena ni haki. Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, atatekeleza maangamizi yaliyoamriwa juu ya nchi yote. Kwa hiyo, hili ndilo Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Enyi watu wangu mkaao Sayuni, msiwaogope Waashuru, wanaowapiga ninyi kwa fimbo na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya. Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma, na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.” BWANA Mwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi, kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu, naye atainua fimbo yake juu ya maji, kama alivyofanya huko Misri. Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu, na nira yao kutoka shingoni mwenu; nira itavunjwa kwa sababu ya kutiwa mafuta. Wanaingia Ayathi, wanapita katikati ya Migroni, wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi. Wanavuka kivukoni, nao wanasema, “Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.” Rama inatetemeka; Gibea ya Sauli inakimbia. Piga kelele, ee Binti Galimu! Sikiliza, ee Laisha! Maskini Anathothi! Madmena inakimbia; watu wa Gebimu wanajificha. Siku hii ya leo watasimama Nobu; watatikisa ngumi zao kwa mlima wa Binti Sayuni, kwa kilima cha Yerusalemu. Tazama, Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, atayakata matawi kwa nguvu kuu. Miti mirefu sana itaangushwa, ile mirefu itashushwa chini. Atakata vichaka vya msitu kwa shoka; Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.

Shirikisha
Soma Isaya 10