Isaya 10:1-4
Isaya 10:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wao wanaotunga sheria zisizo za haki, watu wanaopitisha sheria za kukandamiza. Huwanyima maskini haki zao, na kuwaibia maskini wa watu wangu maslahi yao. Wajane wamekuwa nyara kwao; yatima wamekuwa mawindo yao. Je, mtafanya nini siku ya adhabu, siku dhoruba itakapowajieni kutoka mbali? Mtamkimbilia nani kuomba msaada? Mtakwenda wapi kuweka mali yenu? Litakalowabakia ni kujikunyata kati ya wafungwa na kuangamia pamoja na wanaouawa vitani. Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia, bado ameunyosha mkono wake.
Isaya 10:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao sheria za kudhulumu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang'anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
Isaya 10:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
Isaya 10:1-4 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ole wao wawekao sheria zisizo za haki, kwa wale watoao amri za kuonea, kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyangʼanya yatima. Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu, wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali? Mtamkimbilia nani awape msaada? Mtaacha wapi mali zenu? Hakutasalia kitu chochote, isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka, au kuanguka miongoni mwa waliouawa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.