Isaya 1:13-17
Isaya 1:13-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana; ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, Sabato na mikutano mikubwa ya ibada; sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo moyo wangu wazichukia. Zimekuwa mzigo mzito kwangu, nami nimechoka kuzivumilia. “Mnapoinua mikono yenu kuomba nitauficha uso wangu nisiwaone. Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia, maana mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu. Acheni kutenda maovu, jifunzeni kutenda mema. Tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima, teteeni haki za wajane.”
Isaya 1:13-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mwandamo na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
Isaya 1:13-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
Isaya 1:13-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu. Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia. Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. Mikono yenu imejaa damu; jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu! Acheni kutenda mabaya, jifunzeni kutenda mema! Tafuteni haki, watieni moyo walioonewa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane.