Hosea 6:1-11
Hosea 6:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
“ ‘Twendeni, tukamrudie Mwenyezi-Mungu! Yeye mwenyewe ameturarua, lakini yeye mwenyewe atatuponya. Yeye mwenyewe ametujeruhi, lakini yeye mwenyewe atatibu majeraha yetu. Baada ya siku mbili, atatupa uhai tena, naam, siku ya tatu atatufufua ili tuweze kuishi pamoja naye. Basi tumtambue, tujitahidi kumjua Mwenyezi-Mungu. Kuja kwake ni hakika kama alfajiri, yeye atatujia kama manyunyu, kama mvua za masika ziinyweshayo ardhi.’” Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitakutendea nini ee Efraimu? Nikufanyie nini ee Yuda? Upendo wenu kwangu ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande unaotoweka upesi. Ndiyo maana nimewavamia kwa njia ya manabii, nimewaangamiza kwa maneno yangu, hukumu yangu huchomoza kama pambazuko. Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si tambiko, Kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa. “Lakini mlilivunja agano langu kama mlivyofanya mjini Adamu; huko walinikosea uaminifu. Gileadi ni mji wa waovu, umetapakaa damu. Kama wanyang'anyi wamwoteavyo mtu njiani, ndivyo na makuhani walivyojikusanya na kuvizia. Wanaua watu njiani kuelekea Shekemu, naam, wanatenda uovu kupindukia. Nimeona jambo la kuchukiza sana miongoni mwa Waisraeli: Watu wa Efraimu wanakimbilia miungu mingine naam, Waisraeli wamejitia unajisi. Nawe Yuda hali kadhalika, nimekupangia wakati utakapovuna adhabu.
Hosea 6:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Njooni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga majeraha yetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo nimewakatakata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa. Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana. Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu. Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana. Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi. Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.
Hosea 6:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Njoni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa. Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana. Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu. Na kama vile makundi ya wanyang’anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana. Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi. Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.
Hosea 6:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Njooni, tumrudie BWANA. Ameturarua vipande vipande lakini atatuponya; ametujeruhi lakini atatufunga majeraha yetu. Baada ya siku mbili atatufufua; katika siku ya tatu atatuinua, ili tuweze kuishi mbele zake. Tumkubali BWANA, tukaze kumkubali yeye. Kutokea kwake ni hakika kama vile kuchomoza kwa jua; atatujia kama mvua za masika, kama vile mvua za vuli ziinyweshavyo nchi.” “Nifanye nini nawe, Efraimu? Nifanye nini nawe, Yuda? Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi, kama umande wa alfajiri utowekao. Kwa hiyo ninawakata ninyi vipande vipande kwa kutumia manabii wangu; nimewaua ninyi kwa maneno ya kinywa changu, hukumu zangu zinawaka kama umeme juu yenu. Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu, kumkubali Mungu zaidi kuliko sadaka za kuteketezwa. Wamevunja Agano kama Adamu: huko hawakuwa waaminifu kwangu. Gileadi ni mji wenye watu waovu, umetiwa madoa kwa nyayo za damu. Kama wanyangʼanyi wamviziavyo mtu, ndivyo magenge ya makuhani wafanyavyo; wanaulia watu kwenye njia iendayo Shekemu, wakifanya uhalifu wa aibu. Nimeona jambo la kutisha katika nyumba ya Israeli. Huko Efraimu amejitolea kwa ukahaba na Israeli amenajisika. “Pia kwa ajili yako, Yuda, mavuno yameamriwa.